May 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bei ya Mafuta Kenya yazidi kupaa,zaizidi Tanzania

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli nchini Kenya (EPRA) imetangaza ongezeko jipya la bei ya mafuta, hatua iliyosababisha Kenya kuwa na bei kubwa zaidi za mafuta ukilinganisha na Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Mei 2026, bei ya petroli nchini Kenya imepanda kwa Shilingi za Kenya 16.65 hadi kufikia KSh214.25 kwa lita, sawa na takribani Shilingi za Tanzania 4,300. Dizeli nayo imeongezeka kwa KSh46.29 hadi KSh242.92 kwa lita, sawa na karibu TSh4,860.

Kwa upande wa Tanzania, bei za mafuta zilizotangazwa na EWURA mwezi Mei 2026 zinaonyesha kuwa petroli inauzwa kwa wastani wa TSh4,115 kwa lita huku dizeli ikiwa TSh4,248 katika jiji la Dar es Salaam.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Petroli ya Kenya ni ghali kwa takribani TSh185 zaidi kwa lita ukilinganisha na Tanzania na Dizeli ya Kenya ni ghali kwa zaidi ya TSh600 kwa lita kuliko Tanzania.

Wachambuzi wa uchumi wanaeleza kuwa tofauti hiyo inachangiwa na ongezeko la gharama za mafuta katika soko la dunia, kodi za mafuta nchini Kenya pamoja na gharama za usafirishaji.

Ongezeko hilo linatarajiwa kuongeza gharama za usafiri, bidhaa na huduma nchini Kenya, huku Tanzania ikiendelea kuwa na nafuu kidogo katika sekta ya mafuta ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.