April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asukile, Fully Zullu, Chona kuiongezea makali timu ya Taifa ufukweni

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

NYOTA wanaoshiriki Ligi Kuu Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) Benjamin Asukile, Nurdin Chona wa Tanzania Prisons, Fully Zullu Maganga wa Ruvu Shooting na Ismail Gambo kutoka KMC wameitwa kukiongezea nguvu kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ya Soka la Ufukweni ‘Beach Soccer’.

Kikosi hicho kimeingia kambini kuanza rasmi maandalizi kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) zitakazofanyika kuanzia Mei 23 hadi 29 nchini Senegal.

Tanzania ilifanikiwa kufuzu fainali hizo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kupata ushindi wa jumla wa goli 12-9 wakifanikiwa kushinda goli 8-3 katika mchezo wa kwanza na kufungwa goli 6-4 katika mchezo wa marudiano uliochezwa juzi Aprili 3 kwenye fukwe za Coco.

Wachezaji hao wataungana na Ahmed Juma, Adam Oseja, Erick Manyama, Daniel Mwainyekule, Rolland Msonjo, Jaruph Juma, Ahmad Abdul, Kashiru Juma, Yahya Tumbo, Abdulkadiri Tarib, Steven Mapunda, Said Morad, Ally Daudi, Stanley Mkomola, Hakim Mohammed na Ibrahim Ibadi,

Akizungumzia kambi hiyo, Kocha mkuu wa timu hiyo Boniface Pawasa amesema, tayari alishaandaa mkakati wake na kuja na programu stahiki ambayo itawafanya kuwa bora zaidi katika mashindano hayo.

Amesema, jambo kubwa kwao lilikuwa ni kwanza kufanikiwa kufuzu kwa mara ya pili kushiriki AFCON na baada ya kufanikisha hilo walianza haraka sana kujipanga na kufanyia kazi makosa waliyoyafanya na kuja na mbinu ambazo zitawawezesha kuwa bora zaidi katika maandalizi yao.

Pawasa amesema, katika mashindano hayo wanakwenda kukutana na timu ngumu za bora hivyo ili waweze kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita ni lazima waingie kambini mapema na kufanya maandalizi yatakayowawezesha kuwa bora zaidi kupambana na vigogo wengine waliofuzu kwenye fainali hizo.

Ili kuhakikisha wanakuwa bora zaidi ameamua kuwaongeza wachezaji hao ambao anaamini watawaongezea kitu hasa katika eneo lao la ulinzi na lile la ushambuliaji ambalo lilifanya makosa kadhaa katika mchezo wao wa kuwania kufuzu kushiriki fainali hizo.

Amesema, kambi hiyo itagawanyika katika sehemu tatu ambapo wiki ya kwanza itakuwa kwa ajili ya kujenga utimamu, wiki ya pili itabeba zaidi mambo ya kiufundi huku ile ya tatu ikihusisha zaidi mechi za kirafiki.

“Katika kambi yetu tutajikita zaidi katika mambo makubwa matatu ambayo ni pamoja na kusaka utimamu na katika wiki ya pili ya ufundi tutajikita zaidi kwenye mbinu, ujanja na ubunifu na katika ile wiki ya mwisho ya mechi za kirafiki tutahakikisha tunacheza mechi nyingi za kirafiki ili tuweze kujitathmini kama tumefikia malengo yetu kabla ya kuondoka,” amesema Pawasa.

Kocha huyo amesema kuwa, kitu pekee wanachowaomba Watanzania ni wadau wa michezo ni kuwaunga mkono kwani wana nia ya kwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo na wana nia ya dhati kwani dhamira yao kubwa ni kwenda kuipeperusha vema bendera ya Taifa.

Itakumbukwa kuwa, hivi karibuni kocha huyo aliweka wazi kuwa, ikiwa watatinga katika fainali hizo watahakikisha wanafanya vizuri zaidi ili kupanda zaidi katika viwango vya Afrika na dunia kwani kwa sasa wanashika nafasi ya nane kwa ubora kati ya nchi 52 za Afrika.