May 13, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM Tabora yaanza kusikiliza kero ‘Live’ na kuzitatua

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tabora Mjini kimeanza kusikiliza na kutatua kero za wananchi papo hapo kwa kutumia Wataalamu wa Mipango Miji, Kamishna wa Ardhi na Maafisa Ardhi wa Halmashauri ya Manispaa Tabora.

Akizungumzia kabla ya kuanza zoezi hilo jana Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora Mjini Mohamed Katete alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi ndicho kimepewa dhamana na wananchi kushika dola hivyo kinapaswa kuhakikisha kero zao zote zinasikilizwa na kutatiliwa haraka iwezekanavyo.

Amesema kuwa CCM kupitia ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 kiliahidi kuwa serikali yake itaboresha maisha ya wananchi na kero zinazowakabili zitatatuliwa, hivyo zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji ilani ya uchaguzi.

‘Kila mwananchi mwenye kero ya aina yoyote ile aje Ofisi ya Chama, tutamsikiliza na kutoa maelekezo kwa Wataalamu wetu walioajiriwa na serikali ya CCM ili wayafanyie kazi haraka iwezekanavyo, zoezi hili ni endelevu’, amesema.

Katibu wa CCM Wilaya ya Tabora Mjini Chifu Silvester Yared ambaye ndiye Msimamizi Mkuu wa zoezi hilo ameeleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi kuleta kero zao Ofisi ya Chama na kuahidi kuwa wote watasikilizwa.

Amesisitiza kuwa vikao vyote vya kusikiliza kero hizo vitakuwa chini ya usimamizi wa Chama na wataita Wataalamu wa Idara zote ili kila kero ipatiwe majawabu ya uhakika ili wananchi waendelee kuiamini serikali yao ya CCM.

‘Wataalamu wa Halmashauri ya Manispaa Tabora watakaoelekezwa na Chama kushughulikia kero ya mwananchi fulani waifanye kwa weledi na kwa moyo wa dhati ili mhusika aridhike, kinyume na hapo huyo Mtaalamu hatufai’, amesema.

Baadhi ya Wataalamu walioitwa katika zoezi hilo ni Hussein Sadick (Kamishna wa Ardhi Mkoa), Irene Quambalo (Afisa Ardhi), Mbilinyi (Afisa Mthamini Mkoa), Rogath Joseph, Haruna Maganga (Wapima Ramani) na Issa Lugilimba (Mrasimu Ramani).

Wakiongea kwa niaba ya wananchi wenzao, Stanley Mang’ombe mkazi wa Kata ya Ng’ambo na Paulina Noa mkazi wa kata ya Mtendeni wamekishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kuweka utaratibu huo na kubainisha kuwa wananchi wengi zaidi wataendelee kuipenda CCM.

Wameeleza kuwa jamii ina matatizo mengi kwa sababu Viongozi na Wataalamu wa serikali waliopewa dhamana hawasikilizi na kutatua kero zao kwa wakati ndiyo maana Viongozi wa ngazi za Juu wanapokuja mabango yanakuwa mengi zaidi.