April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asas Azindua kampeni Ismani

Na Zuhura Zukheir, TimesMajira Online, Iringa

MRATIBU wa kampeni Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayewakilisha mkoa wa Iringa Salim Abri (ASAS) amemkabidhi ilani ya uchaguzi mgombea ubunge wa Jimbo la Isimani ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi huku akiwataka wananchi kumpigia kura za heshima mgombea urais wa CCM Dkt. John Magufuli na mbunge wamchague William Lukuvi kutokana na kazi walizozifanya za kuiletea nchi maendeleo.

Mratibu huyo wa kampeni, Salim Asas amesema hayo wakati akizindua kampeni za mgombea ubunge jimbo la Ismani zilizofanyika katika viwanja vya Migoli na kuwa kutokana kazi zilizofanywa na Rais Magufuli akishirikiana na Waziri wa Ardhi ambaye ndie mgombea ubunge wa jimbo la Isimani wananchi wanaombwa kujitokeza kwa wingi oktoba 28 kupiga kura za heshima ili kuwapa moyo wakuendelea kuleta maendeleo.

Asas amesema kuwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kwa mambo aliyoyafanya Rais Magufuli ingekuwa Rais mwingine angefanya kwa miaka 15 hivyo hakuna sababu ya kupoteza kura bali apewe zawadi kwa kupigiwa kura asilimia 100 bila kumsahau mbunge ambaye ni nuru ya Wana-Ismani na Mkoa wa Iringa kwa ujumla.

Amesema wagombea wengi wamekuwa wakipita wakiwadaganya wananchi kuwa wawachague wataleta maendeleo wakati tayari Rais Magufuli ameshafanya mambo makubwa na anahitaji miaka mitano mingine ya kumalizia.

Amesema wananchi wasibabaishwe na mgombea anaekuja na hoja zisizo na mashiko kwani hata wakimchagua watasubiri kwa miaka mingi ndio wapate maendeleo katiak jimbo lao kwa kuwa hana mtandao wa kuwaunganisha wana ismani na maendeleo kama mtandao alionao Lukuvi.

Ameongeza kuwa kutokana na uchapa kazi wa Lukuvi ndani ya jimbo lake na nchi nzima kupitia wizara yake ya ardhi maeneo mbalimbli wamekuwa wakitamani awe mbunge wao na kama katiba ingekuwa inamruhusu basi angekuwa ndani ya miaka mitano anaenda kugombea katika mikoa mingine ili awasimamie hata kwa miezi sita sita tu.

Asas amesema  kuwa kazi zilizofanywa na mbunge wa jimbo la Ismani zinaonekana kwa macho hali inayoifanya CCM kujivunia kuwa na mbunge huyo mkoani wa Iringa kwa kuwa ammaliza migogoro ya ardhi maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Jimboni kwake Ismani ameendelea na zoezi la kusogeza maji karibu ya wananchi umeme huduma ya afya na sekta ya elimu vyote vinapatikana.

Akizungumza, mgombea ubunge wa jimbo la Ismani, William Lukuvi amewataka wananchi kumchagua Rais Dkt John Magufuli na kumchagua yeye kama mbunge pamoja na kumchagua madiwani wa CCM huku akiahidi neema kwa wakazi wa kata ya Migoli kujengwa kituo kikubwa cha afya huku akiwataka kutafuta eneo zuri la kujenga hospitali ambalo halitakuwa mbali na makazi ya watu.

“Tumeamua kujenga hospital yenye chumba cha kuhidhi maiti, itakayokuwa kuwa na huduma zote kama upasuaji ili kuwapunguzia wananchi adha ya kufuata huduma hizo mbali na kwa kufanya hivi tutakuwa tumenusuru maisha ya watu wa hali ya chini mnachotakikwa ni kuamua siku ya tarehe 28 mumpigie kura nani” amesema Lukuvi.

Amesema ili ujenzi wa hospitali hiyo ukamilike kwa haraka anawaomba wakazi wa kata ya Migoli kuhakikisha wanamchagua diwani wa CCM bw. Benito Kayugwa mbunge wa ccm Willium Lukuvi pamoja na Rais wa CCM Dkt. John Magufuli ili kwa kufuata cheni hiyo wapate maendeleo kwa haraka.

Amesema kuwa wananchi wanatakiwa sasa wao kuamua kama wamchague diwani ambaye anauwezo wa kupiga simu muda wowote badala ya kuchanganya madiwani ambao hata kumpigia simu mbunge kueleza jambo wanaogopa.

Mgombea udiwani kata ya Migoli Benito Kayugwa aliwaomba wananchi wa kata ya Migoli kuwa na Imani nae kwa kumpa kura zote za ndio ili akasaidiane na mbunge wa jimbo la Ismani Willium Lukuvi katika kuwaletea maendeleo wakazi wa Migoli ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha afya.

Wakazi wa jimbo la ismani wameishukuru serikali kwa kuwawek katika mpango wa kujengewa hospitali huku wakimuomba Mgombea ubunge na mgombea udiwani kama watapata ridhaa ya kuwaongoza wahakikishe wanakamilisha ahadi yao mara baada ya uchaguzi.

Uzinduzi huo wa kampeni ulipambwa na burudani kutoka kwa wasanii wa kubwa kutoka ndani na nje ya mkoa wa Iringa akiwemo Konde boy pamoja na masai wa Iringa.