Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Airtel Tanzania imezindua mnara mpya wa mawasiliano wenye kasi ya 4G katika kata ya Kayenze, hatua inayolenga kuimarisha ubora wa mtandao na kuondoa changamoto ya mawasiliano hafifu iliyokuwa ikiwakabili wananchi kwa muda mrefu.
Uzinduzi huu ni sehemu ya mkakati wa Airtel Tanzania kusogeza karibu huduma bora za mawasiliano na kifedha kwa wananchi, hususan maeneo yanayokua kwa kasi kiuchumi na kijamii.
Akizungumza May 9, 2026 wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Biashara wa Kanda ya Mwanza Mlaki Mchala amesema Airtel inatambua changamoto ya kipato kwa Watanzania wengi, hivyo inaendelea kuhakikisha huduma zinapatikana kwa gharama nafuu zaidi.
Amesema Airtel imeendelea kuimarisha ushindani katika huduma za Airtel Money kwa lengo la kupunguza gharama kwa wananchi katika matumizi ya kila siku, huku akieleza kuwa kampuni hiyo kwa sasa ni miongoni mwa zenye viwango vya chini vya makato nchini.
“Katika huduma za Lipa, awali wananchi walikuwa wakilalamikia makato makubwa, lakini sasa tumeondoa kabisa makato hayo kwa wateja. Tutaendelea kuboresha huduma hizi kadri mahitaji yanavyoendelea kuongezeka,” alisema.
Mchala amesisitiza kuwa kipaumbele cha Airtel ni kuboresha ubora wa mtandao, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuhakikisha zinamudu gharama kwa wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wake, Mektirida Jacob, Mkazi wa Kayenze amesema ujio wa mnara huo ni faraja kubwa kwa wakazi wa eneo hilo waliokuwa wakikumbana na changamoto ya kukatika kwa mawasiliano.“Kwa sasa tutafaidika vizuri kwa sababu mnara upo karibu nasi. Zamani mtandao ulikuwa unakatika mara kwa mara, lakini sasa hali itakuwa bora zaidi,” amesema.
Ameongeza kuwa wananchi wanatarajia kuendelea kunufaika na maboresho ya huduma pamoja na ofa mbalimbali za mawasiliano kama vile muda wa maongezi, SMS na data.Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kayenze, Yasin Haruna alisema wananchi wa Kayenze wanatoa pongezi kwa Serikali na Airtel kwa kuwaletea huduma hiyo muhimu.
“Tunafurahi sana kuona wamefika hapa kwetu na kutujengea mnara wa mawasiliano. Tunaahidi kuulinda ili uendelee kutoa huduma kwa muda mrefu,” amesema.
Kayenze ni miongoni mwa kata zinazokua kwa kasi ndani ya Ilemela, ikiwa chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. Kata hiyo ina mitaa mitano, kaya 4,187 na wakazi 17,201.Eneo hilo lina shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo uvuvi kutokana na ukaribu na Ziwa Victoria, kilimo cha mbogamboga na biashara ndogondogo, ambazo zote zinategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa mawasiliano ya uhakika.
Katika uzinduzi wa mnara huo, Diwani wa kata ya Kayenze, James Katoro aliwataka wananchi kushiriki katika kulinda miundombinu hiyo muhimu kwa maendeleo ya jamii.“Miundombinu hii inagharimu fedha nyingi, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuilinda ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu,” amesema
Ameongeza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi nchini.

More Stories
Wakazi Nungwi kunufaika na huduma za kidijitali
Mmuya awasili Zimbabwe kuhudhuria mkutano wa Maafa
Aga Khan Hospital yaja na suluhisho ya changamoto ya Uzito uliopitiliza