May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi Nungwi kunufaika na huduma za kidijitali

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas imefungua rasmi duka jipya la huduma katika eneo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kifedha kwa wakazi wa Zanzibar.

Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni eneo la Nungwi – Zanzibar na kuongozwa na Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini A’ Unguja, Nyange Kher Ali, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Nyange ameipongeza Yas kwa kuendelea kuwekeza Zanzibar na kusaidia jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za mawasiliano pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.

“Uwekezaji huu una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wananchi wetu pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu za kidijitali,” amesema Nyange.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja na Uendeshaji wa Yas, Mwangaza Matotola, amesema kufunguliwa kwa duka hilo ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuendelea kuimarisha uchumi wa kidijitali nchini.

“Uzinduzi wa duka hili hapa Nungwi ni sehemu ya mkakati wetu wa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za mawasiliano na kifedha kwa urahisi, haraka na kwa viwango vya hali ya juu,” amesema Matotola.

Amesema, Yas imeendelea kuwekeza katika upanuzi wa miundombinu yake nchini kupitia teknolojia za 4G na 5G, huku kampuni hiyo ikiwa na zaidi ya minara 4,800 inayohudumia zaidi ya wateja milioni 31 Tanzania Bara na Zanzibar.

Matotola amesema, Nungwi ni eneo muhimu kiuchumi kutokana na shughuli za utalii, uvuvi na biashara, hivyo uwepo wa duka hilo utasaidia wananchi na wafanyabiashara kupata huduma kwa ukaribu zaidi.

Aidha, amewahamasisha wananchi kutumia applikesheni mpya ya Yas inayowezesha upatikanaji rahisi wa huduma mbalimbali kidijitali.

Duka la Nungwi linaungana na mtandao wa zaidi ya maduka 556 ya Yas yaliyopo nchini kote, yakilenga kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa Watanzania.