Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Airtel Tanzania imerejea ahadi yake ya kuimarisha ujumuishi wa kifedha na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake, ikilenga zaidi wajasiriamali wadogo wa chakula wanaojulikana kama ‘Mama Lishe’.
Akizungumza mnamo Aprili 25, 2026, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Airtel Money, Meneja wa Uhusiano wa Kimkakati wa Airtel Tanzania, Jemima Masimba,wakati wa msimu wa tatu wa mpango wa ‘Empowering Mama Lishe’ uliofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza.
Hafla iliyowakutanisha Wawakilishi wa Serikali, washiria wa Maendeleo, na Wanawake Wajasiriamali, akiwemo Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha vijana, Zainab Abdallah Issa.
Masimba amesema Airtel Money inaendelea kubuni zana zinazosaidia kuweka akiba kwa usalama na kurahisisha miamala kwa biashara ndogo ndogo.
Amesisitiza umuhimu wa Lipa Namba, akibainisha kuwa inawawezesha wanawake wajasiriamali kupokea malipo kidijitali na kuhifadhi mapato yao kwa usalama.
Amefafanua kuwa kumbukumbu za miamala ya kidijitali zinawasaidia wanawake kujenga wasifu wa kuaminika kifedha (financial credibility), jambo ambalo ni muhimu katika kupata mikopo midogo midogo.”Tunafahamu kuwa wanawake wengi wajasiriamali wanakabiliwa na changamoto za kupata mikopo rasmi kutokana na ukosefu wa dhamana.
Kupitia Lipa Namba, historia ya miamala sasa inaweza kutumika kama kigezo cha uaminifu wa kifedha, hali inayowaruhusu watumiaji sifa za kupata mikopo kulingana na mzunguko wa fedha zao,” amesema Masimba.
Masimba ameongeza kuwa uwekezaji wa Airtel Tanzania katika kukuza ujuzi kupitia ushirikiano wake na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia mfumo wa VSOMO, unatoa kozi za ufundi zikiwemo za mapishi.
“Uwezeshaji wa kiuchumi huenda mbali zaidi ya upatikanaji wa fedha; unahitaji pia maarifa na ujuzi,” alisema. “Tunawahimiza wanawake na vijana kuchangamkia fursa hizi za masomo ili kuimarisha biashara zao.
“Washiriki walieleza jinsi mpango huo ulivyobadilisha maisha yao. Joyce Mmasi wa kikundi cha Bucha Catering Group alisema mpango huo umewasaidia wanawake kutoka kwenye kuhangaika mmoja mmoja hadi kufanya biashara za vikundi zilizopangwa.”Tulikuwa tumetawanyika, kila mmoja akipambana peke yake, mpaka Sarrah Ngoma alipotuunganisha,” alisema.
Ameongeza kuwa msaada wa mitungi ya gesi uliboresha mazingira yao ya kazi na kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni.
Awali akizungumza katika Kongamano hilo,Mbunge Zainab ametoa wito wa kuunganishwa kwa Mama Lishe katika mifumo rasmi ya kiuchumi, akihimiza mafunzo ya mifumo ya ununuzi wa serikali ili kuwawezesha kupata zabuni za umma.
“Nitahakikisha wataalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) wanakuja kutoa mafunzo na kuwaunganisha wanawake hawa kwenye mfumo,” amesema Zainab.
Naye Amina Abdallah wa kikundi cha Stakishari, mjane anayesomesha na aliyejenga chumba kwenye kiwanja chake kupitia biashara hiyo, alisema: “Kupitia biashara hii ya mama lishe, nimefanikiwa kujenga na kumudu elimu ya mwanangu.

More Stories
Hivi hapa vipaumbele nane Wizara ya Madini 2026/27
Airtel yazindua mnara wa 4G Mtwara Vijijini, kuongeza upatikanaji wa intaneti
Wahimizwa kutumia zahanati ya Polisi Mabatini