Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
WANANCHI wanaioshi karibu na zahanati ya Polisi Mabatini iliopo wilayani Nyamagana mkoani Mwanza,wamehimizwa kutumia zahanati hiyo kwa ajili ya matibabu pindi wanapopata changamoto za kiafya.
Zahanati hiyo ya Polisi Mabatini ina inapokea wagonjwa kati ya 60 hadi 100 kwa siku,wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali, huku wajawazito wawili hadi watatu wakijifungulia katika zahanati hiyo kila siku.

Wito huo umetolewa Aprili 25,2026 na Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mabatini, mkoani Mwanza, Mrakibu wa Polisi (SP) Daktari Steven Kisaka, wakati akishiriki kufanya usafi wa mazingira ya zahanati hiyo na wadau wa maendeleo kutoka kikundi cha “Upendo Federation” cha Kata ya Mabatini, kinachojihusisha na huduma mbalimbali za kijamii.
Dk.Kisaka,amesema wataendelea kutoa huduma bora za afya na za uhakika kwa wagonjwa watakaofika katika zahanati hiyo kwa ajili ya kupata huduma za matibabu,wakizingatia weledi wa Jeshi la Polisi.
Mwenyekiti wa kikundi cha Upendo Federation, Seleman Kapera,amesema wamefanya usafi katika zahanati hiyo kwa kutambua kuwa usafi ni afya,hivyo wataendelea na utaratibu huo katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, Polisi Kata ya Mabatini, Mkaguzi wa Polisi (Insp) Shabani Kashakala, amesema tangu kianzishwe kikundi hicho,kimekuwa kikishiriki katika shughuli za usafi wa mazingira na kusaidia kudhibiti uhalifu.
Kashakala amesema kupitia kikundi hicho, wamekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza amani na kuwa wazalendo, hususani kwa vijana ambao wamekuwa mstari wa mbele kujiingiza katika makundi hatarishi.
Zoezi hilo liliambatana na utoaji wa msaada wa sabuni kwa wagonjwa waliolazwa katika zahanati hiyo.



More Stories
Ilemela asilimia 100 kidato cha kwanza waripoti shuleni
Uwekezaji kwa wavulana kujenga uanaume imara
MSD yaboresha huduma Manyoni