March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Silaa amnadi mgombea Udiwani wa CCM Kata ya Zingiziwa

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Ukonga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jerry Silaa, amemnadi na kumuombea kura za ndiyo kwa wananchi wa Kata ya Zingiziwa, Mgombea Udiwani wa Kata hiyo, Selemani Kanniki.

Silaa, amemuombea kura Kanniki,Septemba 20, 2025 kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Kimya Kimya, eneo la Lubakaya, Kata ya Zingiziwa, Jimbo la Ukonga mkoani Dar-es-Salaam.

Amesema, endapo wananchi hao wa Kata ya Zingiziwa yenye takribani wapiga kura zaidi ya 40,000 watamchagua Kanniki, watanufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara kilometa 72 ikihusisha na Zingiziwa.

“Wananchi wa Zingiziwa, naomba msifanye makosa Oktoba 29, 2025,naomba mkafanye chaguo sahihi la kumpigia kura za ndiyo kwa upande wa Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ubunge Jerry Silaa na kwa upande wa Diwani mkamchague Kanniki, ili baada ya hapo twende tukafanye kazi ya kuwaletea maendeleo katika maeneo yenu. Hapa Zingiziwa Kanniki anatosha na anafaa katika kuwatatulia changamoto zenu”, amesema Silaa.

Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa Kata hiyo kupitia CCM, Selemani Kanniki,amesema miradi mingi ya maendeleo katika Kata hiyo, iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita chini ya Dkt. Samia,

Aidha amesema,Serikali chini ya CCM endapo itapata ridhaa ya kushika tena dola,ataiomba kuendelea kuwapelekea miradi ya maendeleo wananchi wa Zingiziwa, ikiwa pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Zingiziwa-Ngomeni, Zogohari- Kwa Ndevu, Nzasa-Somelo na Kariakoo-Mahakamani.

Sambamba na hayo, pia ametoa rai kwa shule zote katika Kata hiyo, kutotoza michango isiyokuwa na tija kwa wanafunzi, akitolea mfano michango ya chakula nk, ambapo amesema hilo ni jukumu la viongozi na Serikali kwa ujumla.