June 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VETA yapongezwa kutoa mafunzo kwa wenye mahitaji maalum

Na Joyce Kasiki,Dodoma

NAIBU  Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Regina Qwaray, ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa mchango wake mkubwa katika kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana na watu wenye mahitaji maalum.

Pongezi hizo amezitoa leo Juni 22,2026 alipotembelea banda la VETA katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Akiwa katika banda hilo,  Qwaray alisema VETA imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaowapa uwezo wa kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

“Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuwaongezea vijana wetu ujuzi. Kupitia mafunzo haya, vijana wanaweza kujiajiri na kujitegemea. Serikali inaendelea kuwekeza zaidi katika kuwawezesha vijana kujiajiri, na lengo hilo litafanikiwa kupitia uwekezaji mkubwa katika vyuo vya VETA,” amesema.

Ameongeza kuwa wahitimu wa elimu ya sekondari na vyuo wana nafasi ya kujiunga na VETA ili kupata ujuzi unaowawezesha kuanzisha shughuli za kiuchumi bila kutegemea ajira za Serikali.

Qwaray pia amesisitiza kuwa maendeleo ya ujuzi kwa wananchi ni moja ya nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

VETA ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza Juni 16, 2026. Maadhimisho hayo yalifunguliwa rasmi Juni 17, 2026 na Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 23, 2026.