June 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRA yawagusa watoto njiti 

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Tanga

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa msaada wa vifaa mbalimbali Hospitali ya Rufaa ya Bombo mkoani Tanga,kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye changamoto mbalimbali, hususani watoto njiti, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya mamlaka hiyo.

Akizungumza jana wakati wa kukabidhi msaada huo, Naibu Kamishna wa Huduma za Kiufundi kutoka Makao Makuu ya TRA, Ted Silkiluwasha,amesema   katika jamii  kuna watu wenye mahitaji maalumu wanaohitaji kusaidiwa, hivyo mamlaka imeona umuhimu wa kuwafikia na kuwasaidia.

Silkiluwasha amesema Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesisitiza  ukusanyaji wa mapato ndio msingi wa maendeleo ya taifa, hivyo ni muhimu kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika safari hiyo,ambapo  Julai 1 mwaka huu mamlaka hiyo itatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake chini ya kaulimbiu ya “Tanzania kwa Pamoja Tunajenga Taifa Letu”.

“Miaka 30 ya TRA imewezekana kutokana na walipa kodi, na mamlaka inatambua kuwa uhai wa walipa kodi ndio uhai wa TRA. Ndiyo maana tumeamua kutoa msaada huu kwa watoto njiti kama sehemu ya kurudisha kwa jamii inayochangia maendeleo ya taifa kupitia kodi,”amesema Silkiluwasha.

 Amesema mamlaka imechagua kufika Hospitali ya Rufaa ya Bombo kwa kuwa ni kituo kinachohudumia watu wenye mahitaji makubwa, ili kuwaonesha kuwa wao ni sehemu muhimu ya jamii.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John,amesema mamlaka hiyo inaamini kila Mtanzania ni mlipa kodi wa sasa au wa baadaye, hivyo hata watoto waliotembelewa ni walipa kodi wa kesho na huenda wakawa watumishi wa baadaye wa  mamlaka hiyo.

Aidha,amewataka wadau na taasisi nyingine mkoani Tanga kujitokeza kusaidia watu wenye uhitaji na kushiriki katika shughuli za kijamii zinazolenga kuboresha maisha yao na kuwapa matumaini.

Akizungumza kwa niaba ya Hospitali ya Rufaa ya Bombo Nuru Omari amesema,hospitali hiyo  hupokea watoto njiti kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga kwa ajili ya matibabu na uangalizi maalum.

Ameeleza kuwa watoto hao hupatiwa huduma mbalimbali, ikiwemo kuongeza kiwango cha sukari mwilini na kusaidiwa kupumua kwa kutumia mashine maalum hadi wanapofikia uzito unaoruhusiwa.

“Mtoto anaporuhusiwa kwenda nyumbani huendelea kufuatiliwa kupitia kliniki maalum ya ukuaji hadi atakapofikia uzito wa kilo tatu, ndipo huendelea na huduma za kawaida za kliniki,”amesema Omari.

Naye Muuguzi Kiongozi wa Wodi ya Watoto wa hospitali hiyo Sister Rukia Mbega, ameishukuru TRA kwa kuguswa na mahitaji ya watoto njiti na kutoa msaada ambao utasaidia kuboresha huduma zinazotolewa kwa watoto hao.

Amesema msaada huo unajumuisha sabuni, nepi (pampers), dawa na makopo ya maziwa ya unga, vitu muhimu vinavyotumika katika malezi na matunzo ya watoto njiti hospitalini.