Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online ,Dodoma
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya, hususan kupitia Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), ambayo kwa sasa imekuwa kitovu cha huduma za kibingwa na kibobezi kwa tiba za mifupa, ubongo, mgongo, na mishipa ya fahamu.
Akizungumza jijini Dodoma na waandishi wa habari , Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alieleza jinsi ambavyo MOI imepiga hatua kubwa za kimaendeleo na kiutendaji katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
“MOI imekuwa mkombozi kwa maelfu ya Watanzania. Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia taasisi hii umeleta mageuzi makubwa ya huduma za afya nchini,” amesema Msigwa.
Amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, MOI imewahudumia jumla ya wagonjwa 849,127, wakiwemo wagonjwa wa nje, wa dharura, na waliolazwa. Kati yao, wagonjwa 37,801 walilazwa na kati ya hao, 32,743 walifanyiwa upasuaji ikiwa ni zaidi ya asilimia 86.6 ya waliolazwa.
Msigwa amesema ,huduma mpya zaidi ya 10 zimeanzishwa, ikiwemo upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu,Matibabu ya kiharusi kupitia mshipa mkubwa wa paja,upasuaji wa nyonga na goti kwa njia ya marudio,kutengeneza viungo bandia kwa teknolojia ya 3D,huduma ya mikono ya bandia ya umeme,upasuaji wa mgongo kwa kutumia njia ya matundu,upasuaji kwa kutumia akili bandia (AI),kliniki za kimataifa kwa wagonjwa maalum.
Aidha amesema ,Taasisi hiyo imeimarisha zaidi huduma za Kibingwa ambapo umefanikiwa kutoa huduma za upasuaji kwa wagonjwa wengi ikiwemo upandikizaji wa nyonga na magoti bandia – idadi 1,487,Upasuaji wa kichwa kikubwa na mgongo wazi kwa watoto idadi 1,890,upasuaji wa ubongo pasipo kufungua fuvu idadi 890,upasuaji wa mgongo idadi 1,184.
Msigwa amesema,katika kuhakikisha huduma bora, Serikali imetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 17.98 kununua na kusimika vifaa vya kisasa kama Mashine za MRI na CT Scan (Bilioni 4.4),vifaa vya upasuaji na mionzi C-arms (Bilioni 2.18),usimikaji wa chumba cha kisasa cha upasuaji wa mishipa ya fahamu Angio Suite (Bilioni 10.1),Magari ya kubebea wagonjwa na vifaa vya ICU (Bilioni 1.3).
Vike vile amesema,Serikali pia imeanzisha na kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ndani ya MOI, ikiwemo ujenzi wa kituo cha kuvunia hewa tiba (oksijeni) kwa gharama ya Sh bilioni 1.5, uliosaidia kuokoa Sh milioni 1.5 kwa siku zilizokuwa zinatumika kununua oksijeni.
Ameitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje (New OPD) kwa gharama ya Sh bilioni 13.8 – ujenzi umefikia asilimia 21.4 ukarabati wa Jengo la Tumaini kwa matumizi ya wagonjwa maalum ukarabati umefikia asilimia 89.
Pia Msigwa amesema ipo Huduma ya Angio Suite, inayotumia teknolojia ya kisasa kufanya upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu huku akisema,huduma hii tayari imeanza na imeleta unafuu mkubwa kwa wagonjwa.
Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) sasa imejitanua kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma za afya barani Afrika ambspo kupitia sera na uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita, MOI imeweza kuokoa maisha, kupunguza rufaa za nje ya nchi, na kuboresha afya ya wananchi kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayopatikana kwenye hospitali kubwa duniani.
“Mageuzi haya ni ishara ya dhamira ya kweli ya Serikali ya Rais Samia katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora ya afya bila kuhangaika,” alihitimisha Msigwa.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi