October 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Rukwa

MADAKTARI Bingwa na Bobezi 29 wamewasili mkoani Rukwa kwa ajili ya huduma za kibingwa kwenye Halmashauri zote za mkoa kwa muda wa siku sita.

Madaktari hao walipokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Msalika Makungu

Makungu aliwakaribisha madaktari hao juzi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Makongoro Nyerere ambao watatoa huduma za kibingwa za Afya na kuwajengea uwezo watoa huduma mkoani humo.

“Tunapo kuja katika mkoa wa Rukwa kwa ajili ya kutoa huduma za afya na kuboresha uwezo kwa watumishi, tunajenga imani kwa wananchi dhidi ya Raisi wetu hivyo niwaombe kuifanya kazi hii kwa uaminifu na kwa bidii.” Alisema

Pia Makungu aliiomba Wizara ya Afya kufanya programu hiyo kwa awamu zinazokuja iweze kufika mpaka katika ngazi ya msingi kwa vituo vya Afya kwani baadhi yake vipo mbali na hospitali za wilaya.

“Utaratibu uliowekea kwa kila robo niombe tupate walau nafasi ya kufika katika vituo vya Afya kwani yapo baadhi ya maeneo ambayo yapo mbali kidogo na Hospitali za Wilaya”, alisema Makungu

Nae Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Ramadhan Masusu alisema mkoa umejipanga vizuri kufanya matangazo kwenye Halmashauri zote wananachi wamesha anza kujiandikisha kwenye hospitali zilizo teuliwa na muitikio wa wananchi ni mkubwa.

“Hivyo ni matarajio yetu wanachi wa mkoa wa Rukwa wataenda kunufaika na ujio wa madaktari bingwa hawa kwani umewarahishia wananchi kutotumia gharama kubwa kufuata madaktari hospiti za Kanda na Taifa.” Amesema