September 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PEPFAR,yapongeza utekelezaji afya za kupambana na UKIMWI Tanga

Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga

Utafiti wa hivi karibuni wa athari za Virusi Vya Ukimwi (VVU), Tanzania 2022-2023 (Tanzania HIV Impact Survey 2022-2023),umeonesha,watumiaji wa dawa za kufubaza Virusi Vya Ukimwi wamefikia asilimia 93.5, mkoani Tanga.

Utafiti huo,umeeleza kuwa hayo yanatokana na jitihada mbalimbali za Serikali pamoja na wadau wa afya mkoani Tanga.Kupitia timu za Mkoa na Halmashauri (R/CHMT) kwa kushirikiana na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS).

Ambapo mradi wa Afya Hatua,unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), kupitia kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa cha Marekani (U.S. CDC),wamekuwa mstari wa mbele kutoa huduma za kinga, matunzo na tiba, kwa watu walio kwenye hatari ya kupata maambukizi na wanaoishi na maambukizi ya VVU.

Hata hivyo,Shirika la THPS limekuwa likishiriki katika utekelezaji wa afua, zinazolenga kutoa kuduma rafiki za VVU kwa vijana, kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.Pia kuhakikisha wapokea huduma wanabaki kwenye huduma na kufubaza VVU.

Hayo yalibainishwa wakati wa ziara ya waandishi wa habari mkoani Tanga, walipotembelea hospitali ya Wilaya ya Korogwe (Magunga ),kituo cha afya St.Raphael pamoja na kituo cha afya cha Mombo vinavyowezeshwa na Shirika la THPS.

Kaimu Mratibu wa kudhibiti UKIMWI (RACC) mkoani Tanga, Judith Kazimoto, amrsema THPS kupitia mradi wa Afya Hatua,wanatekeleza afua mbalimbali za kupambana na VVU, katika vituo 67 vya afya vilivyopo mkoani humo, ikiwemo hospitali ya Mji wa Korogwe.


“Kuanzia Oktoba 2023 hadi Julai 2024, kliniki ya tiba na matunzo ya VVU ya hospitali ya Mji wa Korogwe,ilikuwa na jumla ya vijana 134 wenye umri wa miaka 15 hadi 25, ambao walikuwa wameandikishwa katika huduma za VVU na asilimia 90% ya vijana hao walikuwa wamefubaza makali ya VVU,”amesema Kazimoto.

Ili kuhakikisha huduma bora za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,wajawazito wanaoishi na VVU hupatiwa huduma zote muhimu,na mara baada ya kujifungua, watoto wao usajiliwa na kuchukuliwa vipimo vya VVU mapema.

Kupitia mradi wa Afya Hatua, watoa huduma katika kituo cha Afya cha St. Raphael huhakikisha usajili wa watoto hao unafanyika,wanachukuliwa sampuli za damu ili kufanyiwa kipimo cha VVU, ndani ya wiki sita baada ya kuzaliwa kwao na kuhakikisha wanapatiwa huduma stahiki.

“Kwa kipindi cha kuanzia Oktoba 2023 hadi Julai 2024, jumla ya wapokea huduma za VVU 26 ambao ni wajawazito walijifungua katika kituo hicho. Watoto waliozaliwa na mama hao walisajiliwa ndani ya siku saba baada ya kujifungua. Kati ya hao, 24 sawa na asilimia 93,walichukuliwa vipimo na wote asilimia 100 ,matokeo yalionesha walizaliwa bila maambukizi ya VVU,” amesema Kazimoto.

Kazimoto ameeleza kuwa,kupitia mradi wa Afya Hatua kwa kushirikiana na watoa huduma za afya katika kituo cha afya cha Mombo, wilayani Korogwe, wamehakikisha ufuasi sahihi na kubaki katika huduma za dawa za kufubaza makali ya VVU.Ambapi asilimia 99 ya wapokea huduma 1,501 waliosajiliwa katika kituo hicho wamefubaza VVU.

Mmoja wa wapokea huduma ambaye pia ni mwelimishaji rika, katika kituo cha afya Mombo, Silvia Somi amesema kutokana na huduma anayopatiwa na kufuata masharti anayopewa na wataalam wa afya,afya yake inaendelea kuwa njema,huku akiendelea kuhamasisha wapokea huduma wenzake kubaki kwenye huduma.

“Wengi wanakuja wakiwa wameshakata tamaa,hawaelewi pa kuanzia lakini kutokana na shuhuda ambazo tumekuwa tukiwapatia watu,wengi wamebaki kwenye huduma, tunawatafuta wengine nyumbani na kuhakikisha wanaendelea na huduma ya dawa,”amesema Silvia.

Mratibu wa PEPFAR nchini Tanzania, Jessica Greene,amesema katika kipindi cha miaka 21 iliyopita, Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR imewekeza zaidi ya dola bilioni 7,nchini Tanzania kwa ajili ya kukabiliana na janga la VVU.

“Wakati PEPFAR ilipoanza kazi nchini mwaka 2003, kulikuwa na watu takriban 1,000 waliokuwa kwenye matibabu, lakini kwa sasa tunasaidia watu zaidi ya milioni 1.5 waliopo kwenye huduma ya tiba na matunzo.Huku vifo vinavyotokana na UKIMWI nchini Tanzania vimepungua kwa asilimia 76 tangu mwaka 2023 na maambukizi mapya yamepungua kwa asilimia 58,”amesema Greene.

Greene ameeleza kuwa,serikali ya Marekani inajivunia kushirikiana na Serikali ya Tanzania kufikia malengo ya UNAIDS 95-95-95 ifikapo mwaka 2025.

“Malengo hayo yanalenga asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU kufahamu hali zao, asilimia 95 ya waliogundulika kuwa na VVU wapate matibabu, na asilimia 95 ya wale walio kwenye matibabu waweze kufubaza VVU,”.