November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

bilioni 18.5 kuwezesha wafanyabiashara wadogo

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

SERIKALI imetenga zaidi ya Shillingi Bilioni 18.5 kwaajili ya mikopo yenye riba nafuu kwaajili yakuwawezesha wajasirimali wadogo wakiwemo wanawake.

Hayo yamesemwa Septemba 15, 2023 na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwa ziarani mkoani Mwanza kwenye Kata ya Mondo Wilayani Misungwi.

Naibu Waziri Mwanaidi amesema lengo la Serikali ni kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi hivyo utoaji wa mikopo hiyo itasaidia wajasirimali wadogo hasa Wanawake kupata mitaji itakayowawezesha kuboresha biashara zao.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaid amekipongeza Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi kwa ubunifu wa utengezaji wa mitungi ya maji kwa kutumia saruji ili kuvuna maji ya mvua na kuondokana na changamoto za upatikanaji wa maji katika jamii.

“Hongera sana Mkuu wa Chuo jambo hili ni la kuigwa kwani umeshusha utaalam wa Maendeleo ya Jamii na ufundi kwa wananchi ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili ikiwepo hii ya maji” alisema Naibu Waziri Mwanaidi

Pia Naibu Waziri Mwanaidi amewamasisha Wanawake na Jamii kwa ujumla kushirikiana kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ndani ya jamii hasa kuzingatia Malezi na Makuzi ya Mtoto na kulinda utamaduni wa mtanzania.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Paulo Chacha amesema Wilaya hiyo inaendelea na juhudi mbalimbali za kuhamasisha wananchi kujitolea katika shughuli za maendeleo, ikiwepo ujenzi wa Makazi bora na kupambana na vitendo vya ukatili hasa ndoa za utotoni.

“Mhe. Naibu Waziri huku kwetu wananchi wanahamasika sana kwenye shughuli za maendeleo pia katika kuboresha Makazi kama ulivyojionea mwenyewe lakini tunapambana na vitendo vya ukatili kwa kushirikiana na vikundi mbalimbali hususani vya Wanawake” alisema Chacha.

Akisoma taarifa ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi Mkuu, Charles Achioga amesema Chuo kinashirikiana na jamii ya Wilaya ya Misungwi kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia, ari ya kujitolea katika shughuli za maendeleo na kuibua na kutekeleza miradi mbalimbali katika jamii kwa kutumia wanafunzi wanaosoma na waliohitimu katika Chuo hicho.

Akiwa anaendelea na ziara yake Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea na kukagua ujenzi wa mabweni ya ghorofa mbili lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 352 katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi linalogharimu shillingi milooni 300 na litatatua changamoto za uhaba wa mabweni kwa watoto wa kike Chuoni hapo.

Naibu Waziri Mwanaidi Ali Khamis yupo katika ziara ya kikazi kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa kufuatilia utekelezaji wa Sera Mipango na afua mbalimbali za maendeleo na Ustawi wa Jamii nchini.