Na Joyce Kasiki, Dodoma
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ina imani na Vyama vya Ushirika katika kusimamia matrekta na zana za kilimo ili kuhakikisha zinawanufaisha wakulima katika Kanda zao.
Akizungumza wakati akizindua matrekta hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya kilele cha siku kuu ya wakulima na wafugaji Nanenane katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma Dkt.Samia amesisitiza kuwa matrekta na zana hizo zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, kwa kuwa hatua hiyo itasaidia wakulima kuongeza tija, uzalishaji na kipato, huku akionya dhidi ya matumizi yasiyoendana na malengo ya Serikali.
Rais Samia ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani (NAESA) pamoja na Vyama vya Ushirika.
Alisema Serikali imeamua kutumia Vyama vya Ushirika kama njia muhimu ya kuwafikia wakulima katika maeneo mbalimbali nchini, kutokana na kuwa karibu na wakulima na kufahamu mahitaji yao.
“Sasa tunaanza na nyie, nitakabidhi matrekta yaliyopo hapa yaende yakafanye kazi. Tutaendelea kununua hadi tueneze kama tulivyoahidi,” alisema Rais Samia.
Kwa mujibu wa Rais Samia, awali Serikali ilikuwa na mpango wa kuanzisha vituo vya zana za kilimo katika Kanda mbalimbali nchini, lakini baada ya kutafakari namna bora ya kuwafikia wakulima, ilibaini kuwa Vyama vya Ushirika vina nafasi kubwa katika kusimamia huduma hizo.
Alisema uamuzi huo umetokana na nafasi ya Vyama vya Ushirika katika jamii za wakulima, hivyo kuwawezesha kuwa kiungo kati ya Serikali, zana za kilimo na wakulima wanaozihitaji.
“Nimezindua matrekta kwa ajili ya Vyama vya Ushirika. Mtakumbuka niliahidi kuanzisha vituo vya zana za kilimo katika Kanda zitakazokuwa ndani ya Tanzania nzima,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali imeamua utekelezaji wa mpango huo usimamiwe na Vyama vya Ushirika vya Tanzania katika Kanda zao, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za zana za kilimo kwa wakulima.
Rais Samia alisema Serikali itaendelea kukabidhi matrekta na zana nyingine za kilimo kwa Vyama vya Ushirika ili visimamie matumizi yake na kuhakikisha wakulima katika maeneo yao wanapata huduma kwa wakati.
Alisema lengo la mpango huo ni kuwawezesha wakulima kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa zana za kilimo, kuongeza tija na uzalishaji pamoja na kuinua kipato.
“Tumewakabidhi matrekta haya na zana tutakazonunua kwa Vyama vya Ushirika ili wao wawasimamie wakulima wao,” alisema Rais Samia.

More Stories
Ndejembi amtaka Mkandarasi kuongeza kasi ujenzi wa Barabara ya Kahama
Wakulima Mbarali watakiwa kutanua Kilimo cha Korosho
COSTECH yapongeza Mbunifu wa zana za Kilimo