August 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wapewa mbinu kukabiliana na Sumukuvu

Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline

MKURUGENZI wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, (GCLA) Daniel Ndiyo, amewataka wananchi kutumia maabara za mamlaka hiyo kuchunguza mazao ya kilimo ili kubaini usalama wake kabla ya kutumika au kuuzwa.

Ndiyo ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma.

Amesema wakulima wanapaswa kupeleka mazao yao kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi ili kuthibitisha kama ni salama kwa mlaji, hatua ambayo itawasaidia kuchukua hatua stahiki kabla ya kuyapeleka sokoni.

“Unaweza kuwa na mazao yako kabla hujataka kuuza, njoo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali tuchunguze kama ni salama kwa mlaji, jambo linalomsaidia mkulima kuchukua hatua stahiki,” amesema Ndiyo.

Aidha, amewataka wakulima kuzingatia mbinu za kitaalamu wakati wa uvunaji na uhifadhi wa mazao ili kujikinga na tatizo la sumukuvu.

Amesema ni muhimu kuepuka tabia ya kurundika mazao katika makundi wakati wa mavuno na badala yake kutumia mbinu za kisasa za kuhifadhi ili kuhakikisha mazao yanabaki salama kwa matumizi.