August 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uzalishaji mbegu bora waongezeka kwa asilimia 55 nchini

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline, Dodoma 

 TAASISI ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imesema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika tasnia ya mbegu, hatua iliyowezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu bora, kuboresha miundombinu ya maabara na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Agosti 7,2026,Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI Nyasebwa Chimagu kuhusu Utekelezaji wa mwaka 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27 ambapo amesema  mafanikio hayo yametokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Kilimo, ambapo bajeti ya sekta ya mbegu imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 16.79 mwaka 2021/2022 hadi Shilingi bilioni 85.15 mwaka 2025/2026, sawa na ongezeko la asilimia 307.

Chimagu amesema uzalishaji wa mbegu zilizothibitishwa ubora umeongezeka kutoka tani 50,750 mwaka 2021/2022 hadi tani 78,842 mwaka 2025/2026, sawa na ongezeko la asilimia 55.35. Kati ya mbegu hizo, tani 45,101 zimezalishwa nchini kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na kampuni binafsi, huku tani 33,741 zikiagizwa kutoka nje ili kukidhi mahitaji ya soko.

Aidha, Serikali kupitia mpango wa ruzuku ya mbegu bora za mahindi imesambaza tani 42,850.19 zenye thamani ya Shilingi bilioni 333.28 kwa wakulima nchini, ambapo Shilingi bilioni 68.75 zimetolewa na Serikali kama ruzuku na Shilingi bilioni 264.54 zimechangiwa na wakulima. TOSCI imesema hatua hiyo imechangia Tanzania kuendelea kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 130 pamoja na kuimarisha uzalishaji wa mazao ya biashara.

Katika kuimarisha huduma za uthibiti wa ubora wa mbegu, TOSCI imeeleza kuwa Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 7.23 katika ujenzi na ukarabati wa maabara za kisasa za mbegu Morogoro, Mwanza, Tabora na Mtwara pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya maabara vinavyokidhi viwango vya kimataifa.

Kwa upande wa ubunifu wa teknolojia za mbegu, taasisi hiyo imesema katika mwaka 2025/2026 zimesajiliwa aina mpya 113 za mbegu za mazao mbalimbali ikiwemo mahindi, mtama, muhogo, alizeti, tumbaku, ndizi, parachichi na mazao ya bustani. Hatua hiyo imefanya Tanzania kuwa na jumla ya aina 1,318 za mbegu zilizosajiliwa kwa matumizi ya wakulima na biashara.

TOSCI pia imebainisha kuwa imeendelea kudhibiti biashara ya mbegu zisizokidhi viwango kwa kufanya ukaguzi katika maduka, maghala na viwanda vya mbegu nchini. Katika mwaka 2025/2026, watu 22 walichukuliwa hatua za kisheria kutokana na kukiuka Sheria ya Mbegu, ikiwa ni sehemu ya kulinda maslahi ya wakulima na kuhakikisha mbegu bora pekee zinafika sokoni.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, Tanzania imeendelea kufanya vizuri kimataifa katika tasnia ya mbegu kwa kushika nafasi ya tatu barani Afrika kwa ubora wa sekta ya mbegu, huku ikiendelea kuwa miongoni mwa nchi 14 za Afrika zenye maabara zilizoidhinishwa na International Seed Testing Association (ISTA). Aidha, mwaka 2025/2026 vibali 392 vilitolewa kwa ajili ya kuuza tani 993.21 za mbegu nje ya nchi, hatua inayochochea biashara na upatikanaji wa fedha za kigeni.

Kwa mwaka 2026/2027, TOSCI imejipangia kuongeza upatikanaji wa mbegu bora zilizothibitishwa ubora hadi tani 105,000, kukamilisha miradi ya maabara mpya, kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma, kuvutia uwekezaji zaidi katika tasnia ya mbegu na kuendelea kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa kimataifa ili kuongeza ushindani wa mbegu za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.