Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
NDOTO ya mkazi wa Vikindu, Mohammed Misanga, ya kuboresha huduma za afya katika jamii yake imepata msukumo mpya baada ya kujishindia shilingi milioni 50 kupitia kampeni ya “Kila Muamala ni Bao la Ushindi” iliyoendeshwa na Mixx kwa ushirikiano na Hisense.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kampeni na kukabidhi zawadi kuu, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Angelica Pesha, amesema washindi wa mwaka huu walionyesha jinsi huduma za kifedha kidijitali zinaweza kuwa chachu ya kutimiza ndoto na kubadilisha maisha ya watanzania wanaoendelea kutumia huduma hizo.

“Hii imekuwa ni zaidi ya kampeni, tumeona ndoto za wateja wetu zikitimizwa. Kila mshindi alieleza jinsi ushindi wake ulivyobadilisha maisha – kuna walioongeza mitaji, kuna waliolipa ada, kuna waliosafiri nje ya nchi kwa mara ya kwanza na kuna walioweza kujikimu kimaisha.
“Kampeni imegusa maisha ya washindi, familia zao na jamii zinaozowazunguka. Hii ndiyo maana halisi ya kauli mbiu yetu ya ‘Kila Muamala ni Bao la Ushindi’,” amesema Pesha.
Amefafanua kuwa, kampeni hiyo ya takribani miezi miwili ilianzishwa kwa lengo la kusherehekea Kombe la Dunia na watanzania huku Mixx ikihamasisha matumizi ya huduma za kifedha kidijitali kwa wateja wake.
Watanzania zaidi ya 100 walinufaika kwa kujishindia zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu,vifaa vya kielektroniki kutoka Hisense pamoja na safari ya kwenda Mexico kushuhudia michuano ya Kombe la Dunia.

“Tumeona ongezeko la matumizi ya huduma za Mixx, ambapo maelfu ya miamala ilifanyika kupitia huduma mbalimbali katika kipindi chote cha kampeni zikiwemo huduma za kutuma na kupokea fedha, kulipa bili, kufanya malipo kwa wafanyabiashara kupitia Lipa kwa Simu, kuwekeza na kutumia Mixx Super App.
“Tunaahidi kuendelea kuwa wabunifu na kuleta suluhisho zinazorahisisha maisha ya Watanzania,” amesema.
Aidha, ameshukuru Hisense kwa ushirikiano katika kampeni hiyo pamoja na wateja wa Mixx, vyombo vya habari, watayarishaji wa maudhui na wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa mchango wao ulioiwezesha kampeni kufikia mafanikio yaliyokusudiwa.

Akizungumza kwa niaba ya Hisense, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Mars Communications, Tahera Karim, amesema ushirikiano kati ya Hisense na Mixx umeonesha jinsi sekta binafsi zinavyoweza kushirikiana na kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania kupitia kampeni zinazogusa maisha ya wananchi.
“Tangu mwanzo wa kampeni hii tulikuwa na lengo la kusherehekea na wateja wetu kwa kuwapatia zawadi zenye thamani, lakini leo tunafurahi kuona zawadi hiyo ikigeuka kuwa chanzo cha matumaini kwa jamii.
“Ndoto ya Mohammed ya kujenga kituo cha afya inaonesha kuwa ushirikiano wetu na Mixx umeweza kuzalisha matokeo yanayovuka mipaka ya biashara na kugusa maisha ya watu,” amesema Karim.
Kwa upande wake, mshindi wa zawadi kuu ya Shilingi milioni 50, Mohammed Misanga, alisema hadi kufikia siku ya jana alikuwa bado haamini kama kweli ameshinda, akieleza kuwa mara baada ya kutangazwa mshindi alihisi kama anaota na si jambo la kweli.
Mohammed Misanga alisema sehemu ya fedha hizo ataielekeza katika kuwahudumia wazazi wake pamoja na kutimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kuanzisha kituo cha afya .

“Nawashukuru sana Mixx na Hisense kwa kuandaa kampeni hii ambayo imebadili maisha yangu.
“Kupitia ushindi huu, sasa nina fursa ya kutimiza ndoto yangu ya muda mrefu ya kujenga kituo cha afya kitakachowahudumia wakazi wa Vikindu na maeneo ya jirani.
“Ninaamini kituo hiki kitasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya katika eneo letu,” amesema Mohammed Misanga.

More Stories
Watanzania zaidi ya 90 wanufaika ‘ ikiingia tu goli’
Yas yazindua msimu wa sita Zanzibar Marathon 2026
Tamasha kuhamasisha mapambano dhidi dawaza za kulevya lafana