October 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania mwenyeji mkutano wa COP12

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Dar

TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), utakaofanyika kuanzia Oktoba 6 hadi 9, mwaka huu katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar-es-Salaam, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuufungua.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es-Salaam Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni amesema,washiriki 700 wanatarajiwa kutoka nje ya nchi na wengine 1,461 kutoka ndani ya nchi.

Amesema,mkutano huo utakuwa na kaulimbiu isemayo: “Kuelekea Uchumi wa Buluu Endelevu katika Ukanda wa Magharibi wa Bahari ya Hindi kwa Manufaa ya Watu na Mazingira ya Asili: Safari ya Miaka 40,” huku ajenda kuu zikiwa ni pamoja na kudhibiti uchafuzi wa bahari na pwani unaotokana na shughuli za nchi kavu na baharini, ushirikiano wa kikanda katika usimamizi wa mifumo ya ikolojia na rasilimali zinazovuka mipaka, ikiwemo uvuvi na maeneo ya hifadhi.

“Katika mkutano huo pia tutajadili mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kuongeza ustahimilivu wa jamii, miundombinu na mifumo ya ikolojia ya pwani, huku uhifadhi wa bioanuai ukilenga kulinda mikoko, matumbawe, nyasi bahari na maeneo muhimu ya ikolojia”amesema

Amesema mkutano huo pia utajadili namna ya kukuza uchumi wa buluu kwa kuunganisha uhifadhi wa mazingira na fursa za uwekezaji, biashara, ajira na maendeleo ya jamii.

Pia amesema,sayansi na teknolojia ni miongoni mwa maeneo yatakayojadiliwa, ikiwemo kuimarisha matumizi ya Marine Spatial Planning (MSP) na kujenga msimamo wa pamoja katika masuala ya kimataifa kama usimamizi wa anuwai ya kibiolojia nje ya mamlaka ya kitaifa (BBNJ).

Hata hivyo amesema,mkutano huo unatarajiwa kupitisha maamuzi ya Nchi Wanachama, Joint Ministerial Declaration pamoja na kufanya uchaguzi wa Baraza la Viongozi kwa kipindi cha miaka miwili 2026 hadi 2028.

Kwa mujibu wa Masauni, Tanzania kuwa mwenyeji wa COP12 kunaleta matarajio makubwa, ikiwemo kuimarisha diplomasia ya mazingira, kutolewa kwa Azimio la Dar-es-Salaam (DSM), pamoja na kuvutia fedha, teknolojia na uwekezaji kutoka mifuko ya kimataifa.

Aidha amesema,fursa za kiuchumi zitakazopatikana ni pamoja na kuwaunganisha wawekezaji katika sekta za uvuvi, utalii wa baharini, kilimo cha mwani na bioeconomy, huku jamii za pwani zikitarajiwa kunufaika kupitia uvuvi endelevu, aquaculture (ufugaji wa viumbe maji) na kuongeza thamani ya mazao.

Amesema Tanzania tayari imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuanzisha Kitengo Mahsusi cha Kuratibu Maendeleo ya Uchumi wa Buluu, huku kupitia Mkataba wa Nairobi na Mkakati wa Uchumi wa Buluu jamii za pwani zikinufaika na miradi ya kipato, uhifadhi shirikishi, usafi na miundombinu pamoja na ushiriki wa wanawake.

Ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na usimamizi endelevu wa rasilimali katika maeneo ya Mkinga na PECCA, kurejesha misitu ya mikoko katika Delta ya Rufiji, ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya ukusanyaji na usafishaji wa maji machafu Chake Chake, Pemba, pamoja na udhibiti wa taka za plastiki.

Ameongeza kuwa kumekuwa na kuongezeka kwa mafunzo na ushirikishwaji wa wanawake katika shughuli za usimamizi na urejeshaji wa mazingira.

Aidha ametoa wito kwa Wizara, Taasisi za Umma, Sekta Binafsi, wanazuoni, watafiti, mashirika ya kiraia na wananchi wote kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya mkutano huo ili kuleta tija na maendeleo endelevu kwa Taifa.