October 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mzozo Mashariki ya Kati wapandisha bei za mafuta

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema inaendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha bidhaa za mafuta zinapatikana nchini kwa uhakika na kwa bei himilivu, licha ya mabadiliko ya bei katika soko la dunia yanayoendelea kuathiri bei za ndani.

Hatua hizo zimechukuliwa  kutokana na mwenendo wa bei za mafuta nchini kuendelea kuathiriwa na mgogoro wa kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati, ambako Tanzania hununua sehemu kubwa ya bidhaa zake za mafuta, ambao uliibuka upya na kuathiri uzalishaji, upatikanaji na usafirishaji wa mafuta duniani hali hiyo ilisababisha kupanda kwa bei za bidhaa za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia.

Kutokana na mwenendo huo, bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini kwa mwezi Oktoba 2026 zimeongezeka ikilinganishwa na Septemba 2026, baada ya bei hizo kushuka kwa miezi mitatu mfululizo.

Kufuatia hali hiyo , Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli zitakazotumika nchini kuanzia Jumatano, Oktoba 7, 2026, saa 6:01 usiku.

Kwa mwezi Oktoba 2026, mkoani Dar es Salaam, bei kikomo ya rejareja ni Sh.4,057 kwa lita ya petroli, Sh.4,086 kwa lita ya dizeli na Sh.4,067 kwa lita ya mafuta ya taa.

Mkoani Tanga, bei kikomo ya rejareja ni Sh.4,123 kwa lita ya petroli, Sh.4,152 kwa lita ya dizeli na Sh.4,133 kwa lita ya mafuta ya taa.

Mkoani Mtwara, bei kikomo ya rejareja ni Sh.4,170 kwa lita ya petroli, Sh.4,199 kwa lita ya dizeli na Sh.4,180 kwa lita ya mafuta ya taa.

Kwa mujibu wa taarifa ya EWURA, wananchi wametakiwa kuhakikisha wanachukua risiti kila wanaponunua mafuta katika vituo vya mafuta ili kuwa na ushahidi wa ununuzi huo.