September 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaeleza mkakati kuendeleza michezo,wenye ulemavu


Na Joyce Kasiki, Dodoma


SERIKALI imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuendeleza michezo kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo kuandaa makocha, kuendesha mashindano ya ndani na kuwezesha wanamichezo wenye ulemavu kushiriki mashindano ya kimataifa.


Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Nyamizi Simon Mhoja, lililohusu mkakati wa Serikali wa kuendeleza michezo kwa watu wenye ulemavu pamoja na kuzalisha wachezaji wenye ulemavu.


Waziri Makonda amesema Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imekuwa ikihamasisha na kuendeleza ushiriki wa watu wenye ulemavu katika michezo kwa kuandaa makocha wa michezo ya watu wenye ulemavu na kuendesha matamasha ya michezo yanayowajumuisha.


Amesema Serikali pia imekuwa ikiendesha mashindano ya ndani katika michezo mbalimbali kwa watu wenye ulemavu, pamoja na kuwezesha wanamichezo hao kushiriki katika mashindano ya kimataifa.


Kwa mujibu wa Waziri Makonda, Serikali kupitia BMT imeendelea pia kuhamasisha uanzishaji na usajili wa vyama vya michezo kwa watu wenye ulemavu ili kusaidia kusimamia maendeleo ya michezo hiyo.


Amesema hadi Agosti 2026, jumla ya vyama tisa vya michezo kwa watu wenye ulemavu vimesajiliwa, vikiwemo vyama vinavyosimamia michezo ya soka, mpira wa kikapu, tenisi, riadha na kuogelea.


Mbunge Mhoja aliitaka Serikali kueleza mkakati ilionao wa kuendeleza michezo kwa watu wenye ulemavu pamoja na namna inavyolenga kuzalisha wachezaji wenye ulemavu.