Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA), imepunguza masharti ya uwekezaji wa vituo vya mafuta maeneo ya vijijini, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati salama na kukomesha biashara holela ya mafuta kwenye chupa na vidumu ambayo ni hatari kwa wananchi,mali na mazingira.
Hivyo EWURA Kanda ya Ziwa imewahamasisha wawekezaji kuwekeza katika vituo vya mafuta maeneo ya vijijini kwani imeweka utaratibu rahisi unaolenga kupunguza gharama na kuondoa changamoto zilizokuwa zikikwamisha uwekezaji huo.

Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Nyirabu Musira, amesema hayo Agosti 3, 2026 wakati akizungumza katika banda la mamlaka hiyo kwenye maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yanayoendelea katika viwanja vya Nyamh’ongolo wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.
Musira,amesema ushiriki wa EWURA katika maonesho hayo unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma wanazodhibiti, kusaidia waombaji wa leseni kufahamu taratibu zinazohitajika, pamoja na kupokea na kufanyia kazi malalamiko ya watumiaji wa huduma hizo.
“Pia tunatoa maelezo kwa wawekezaji watarajiwa wanaotaka kuwekeza katika huduma tunazosimamia, ili waweze kufahamu taratibu na mahitaji muhimu.Moja ya maeneo ambayo tumeweka mkazo katika maonesho haya ni uwekezaji wa vituo vya mafuta vijijini, kutokana na changamoto ya baadhi ya wananchi kuona kuwa ujenzi wa vituo hivyo unahitaji gharama kubwa,”amesema Musira.
Amesema mamlaka hiyo imefanya maboresho mbalimbali ili kuwawezesha wawekezaji kuanzisha vituo hivyo, ikiwemo kupunguza gharama za maombi ya leseni kutoka sh.milioni 5 hadi sh.milioni 1 huku miundombinu ya vituo vya mafuta vijijini haitalazimika kufanana na ile ya mijini.
“Kwa kijijini kituo cha mafuta chenye pampu moja au kinachouza bidhaa moja tu kinaweza kupewa leseni ili kiweze kuhudumia wananchi wa maeneo hayo.Pia masuala ya mazingira, mwombaji anaweza kutumia kibali kutoka kwa Maofisa Mazingira wa halmashauri husika, ambacho kitazingatiwa wakati wa mchakato wa utoaji wa leseni,”amesema.
Pia amesema maeneo mengi ya vijijini ambayo hayajapimwa yanaweza kuruhusiwa endapo mwekezaji atawasilisha hati ya ruhusa kutoka kwa mamlaka husika ya kijiji au mtaa inayomruhusu kujenga kituo hicho.

Musira amesema,hatua hiyo inalenga kupunguza biashara holela ya uuzaji wa mafuta katika maeneo yasiyo na vituo rasmi, ambako baadhi ya watu huuza mafuta kwenye chupa na vidumu bila kuzingatia usalama.
Amesema mafuta ya petroli ni bidhaa yenye hatari ya kulipuka na kusababisha madhara kwa maisha ya watu, mali na mazingira, hivyo uwepo wa vituo rasmi katika maeneo ya vijijini utasaidia kuongeza usalama na upatikanaji wa huduma hiyo.


More Stories
TARI-Ukiriguru yaongeza tija kwa wakulima
NIRC yatangaza neema kwa Wakulima Nanenane
DCEA yateketeza hekari 3,117.9 mashamba ya bangi Lindi