July 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara watakiwa kushiriki kampeni ya usafi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Dar

WAFANYABIASHARA wilayani Ilala wametakiwa kushiriki kampeni ya Serikali ya usafi kwa ajili ya kulifanya Jiji la Dar-es-Salaam  liwe na madhari ya kupendeza na  kuvutia.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward  Mpogolo,amezungumza  Julai 25,2026 wakati wa kampeni endelevu ya usafi wa mwisho wa mwezi ambao imewashirikisha watumishi wa halmashauri  hiyo pamoja na kampuni za usafi ikiwemo SATEK na JUZA.

Ambapo amewataka wafanyabiashara waliopo wilayani Ilala kushirikiana na Serikali kuhamasisha kampeni hiyo ya usafi katika maeneo yao ya biashara kila wakati hususani kila jumamosi.

Huku akizitaka  na kampuni za usafi  kuhakikisha wana timiza  wajibu wao kwa kuondoa taka kwa wakati ili kuepuka mrundikano wa taka mbele ya maduka na biashara.

Amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya hautakuwa na tija ikiwa wananchi hawatazingatia usafi wa mazingira wanayoishi pamoja na yale wanayofanyia kazi.

“Afya bora huanzia kwenye kinga huku usafi ukiwa nguzo muhimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa.Nawashukuru  Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa kujitolea kwenu,naomba mitaa yote iliopo Ilala iwe safi  kwa kuendeleza kampeni hii ya usafi ya Serikali  kwa kufanya usafi kila siku na kushiriki usafi wa mwisho wa mwezi pamoja na  wananchi,”amesema Mpogolo.