September 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rashal yaharakisha Ujenzi wa Bomba la Gesi Kisemvule Mbagala

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

UJENZI wa bomba la gesi asilia lenye urefu wa kilomita 22 kutoka Kisemvule hadi Mbagala umeingia hatua muhimu, huku kampuni ya Rashal Energies Limited ikiongeza kasi ya kazi katika maeneo ya njia yanayoweza kuathiriwa zaidi na mvua kubwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Rashal Energies Limited, Farhiya Warsame, mradi huo unaendelea kwa wakati na ratiba ambapo unatarajiwa kukamilika Januari 2027, huku timu za ujenzi zikielekeza nguvu katika eneo la kuvuka Mto Mzinga na Vikundu Marsh, kabla ya kuanza kwa mvua zinazotarajiwa za El Niño.

Ujenzi wa bomba hilo ulianza rasmi Julai 28, 2026, baada ya vibali na idhini zote za kisheria kukamilishwa Mei mwaka huu na timu za ujenzi kuanza maandalizi na kuhamasishwa Juni.

Warsame amesema hadi sasa takribani kilomita mbili za bomba zimeunganishwa, huku kilomita 1.5 zikiwa zimechimbwa mitaro. Sehemu zilizokamilika zimekwishawekwa kwenye mitaro, kufunikwa na kufanyiwa majaribio ya shinikizo.

Mradi huo unafadhiliwa kikamilifu kwa mtaji wa Watanzania na unatekelezwa na wataalamu na wakandarasi wa Kitanzania, kwa mujibu wa kampuni hiyo.

Baada ya kukamilika, bomba hilo litaunganisha zaidi ya viwanda 10 vilivyopo katika ukanda wa Kisemvule–Mbagala na gesi asilia inayosafirishwa kwa mabomba, kutoa huduma kwa kituo cha Dar es Salaam Rapid Transit (DART) Mbagala na kuwa msingi wa kituo kikuu cha CNG kitakachosaidia upanuzi wa mtandao wa gesi hiyo katika jiji la Dar es Salaam.

Aidha Warsame, amesema mradi huo umeandaliwa kuonyesha uwezo wa kampuni za Kitanzania kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya nishati kwa viwango vya kimataifa.

“Bomba hili linafadhiliwa na Watanzania, linaandaliwa kitaalamu na Watanzania na linajengwa na Watanzania kwa manufaa ya viwanda na kaya za Watanzania,” amesema Warsame.

Amesema mradi huo pia unalenga kujenga kizazi kipya cha wataalamu wa Kitanzania ambao wataweza kushiriki katika miradi mingine ya miundombinu ya gesi nchini.

Kwa mujibu wa Warsame, zaidi ya kujenga miundombinu, kampuni inawekeza katika kuwajengea uwezo mafundi wa kuchomelea mabomba, wapima ardhi na wahandisi wa Kitanzania, ambao ujuzi wao utaendelea kutumika katika miradi ya usambazaji wa gesi nchini kwa miaka ijayo.

Bomba hilo linatarajiwa kuwa na nafasi muhimu katika upanuzi wa miundombinu ya gesi asilia iliyobanwa (CNG) jijini Dar es Salaam.

Katika awamu ya kwanza, Kituo Kikuu cha CNG Mbagala (Mother Station) kitabanisha gesi moja kwa moja kutoka kwenye bomba kwa ajili ya kujaza magari.

Aidha, Kituo cha Vijibweni (Daughter Station) kitahudumiwa kwa kutumia malori maalumu ya kubeba gesi iliyobanwa, kwa lengo la kuhudumia eneo linalokua kwa shughuli za viwanda kuzunguka Kigamboni.

Awamu ya pili ya mradi inatarajiwa kuhusisha ujenzi wa vituo vingine vitano vya CNG katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, hatua inayolenga kuweka msingi wa mtandao mpana wa CNG katika jiji hilo.

Maendeleo hayo yanaweza kuongeza matumizi ya gesi asilia katika sekta ya usafiri, wakati Tanzania ikiendelea kutafuta njia za kuongeza matumizi ya nishati safi na yenye gharama nafuu zaidi.

Bomba hilo linajengwa katika maeneo yenye shughuli nyingi za kibinadamu, ambako tayari kuna miundombinu ya maji, umeme na mawasiliano, jambo linalohitaji umakini mkubwa wa kiufundi.

Mhandisi wa Bomba wa Rashal Energies Limited, Peter Shauribosho, amesema hadi sasa mradi huo haujasababisha uharibifu wa miundombinu ya wahusika wengine katika njia inayopita bomba hilo na hakuna kiunganishi cha bomba kilichokamilika ambacho kimelazimika kufanyiwa kazi upya.

“Kufanya kazi katika korido yenye shughuli nyingi kama Kisemvule–Mbagala hakutupi nafasi ya kufanya makosa. Kila kiunganishi tunachofanya lazima kiwe sahihi mara ya kwanza,” amesema Shauribosho.

Amesema timu za ujenzi kwa sasa zinaweka mkazo katika maeneo ya Mto Mzinga na Vikundu, kutokana na uwezekano wa maeneo hayo kuathiriwa zaidi na mvua.

Shauribosho amesema timu maalumu zimepelekwa katika maeneo hayo kuhakikisha kazi muhimu inakamilishwa kabla ya kuanza kwa mvua, huku kampuni ikiwa na matumaini ya kukabidhi bomba lililokamilika na kufanyiwa majaribio ya shinikizo ifikapo Januari 2027.
Mradi huo pia unaendana na juhudi za Serikali za kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Warsame amesema bomba hilo limebuniwa kwa kuzingatia uwezekano wa kuunganisha kaya katika siku zijazo na kusaidia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Mei 2024, ambao unalenga kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Gesi asilia itakayotumika katika bomba hilo itatolewa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Kwa Tanzania, umuhimu wa mradi huo hauishii katika kusafirisha gesi kutoka Kisemvule kwenda Mbagala. Miunganisho ya viwanda, miundombinu ya CNG na uwezekano wa kuunganisha kaya vinaifanya bomba hiyo kuwa sehemu ya juhudi pana za kuongeza matumizi ya gesi asilia katika uchumi wa ndani.

Iwapo itakamilika kama ilivyopangwa, mradi huo utaunganisha kwa karibu zaidi rasilimali ya gesi asilia ya Tanzania na usafiri wa mijini, viwanda na kaya, huku ukitoa mfano wa nafasi inayoongezeka ya mtaji na utaalamu wa Watanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya nishati.