June 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kihongosi:Msibebe ajenda za Watu ambao familia zao zipo nje ya Nchi

Na Agnes Alcardo, Timesmaira Online. Arusha

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapjnduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amezindua Shina la Wakereketwa Arusha Noah Saccos, lililopo Stendi kuu Arusha na kuwasihi wananchi wa Arusha kutowasikuliza wanasiasa wanaochochea maandamano.

Kihongosi amesema hayo leo Juni 6, 2026 alipokuwa akizungumza na wanachama wa shina hilo pamoja na wananchi wa Arusha, akisema kuwa kumekuwa na wanasiasa wanaotumia lugha chafu na kuhamasisha maandamano jambo ambalo si zuri kwa ustawi wa jamii na nchi nzima.

Kihongosi, amewataka wananchi hao kuzipuuza ajenda za wanasiasa hao, akisema kuwa wanasiasa hao wamekuwa wakihamasisha machafuko kwa maslahi yao binafsi, huku akiwataka vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa kutojikita katika ajenda za kuharibu amani na badala yake wajikite kujenga uchumi wao.

Aidha, amewataka wananchi wote kwa ujumla kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akiielezea miradi ya kimkakati iliyokamilika chini ya uongozi wa Rais samia.

Pia amesema, wananchi wa Arusha wanapaswa kutembea kifua mbele kutokana na kuendelea kupokea fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo Sh. Bil 520 walizopatiwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji ambao tayari umekamilika.

Awali, Kihongosi akiendelea na ziara yake mkoani Arusha, leo ameingia katika Wilaya ya Arusha Mjini, ambapo alipokelewa katika Ofisi za CCM katika wilaya hiyo.

Kihongosi leo anamaliza ziara yake ya siku tatu mkoani Arusha, kwa kutembelea miradi ya maendeleo, kukagua uhai wa chama kupitia mashina na kusikiliza na kutatua kero za wananchi kupitia mkutano wa hadhara.