June 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kihongosi ahimiza ulipaji ada ya uanachama

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Arusha
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kenani Kihongosi, ametoa wito kwa wanachama wa Shina namba nne, Tawi la TFA, Kata ya Karatu kuendelea kulipa ada ya chama kama chama hicho kinavyoelekeza.

Rai hiyo imetolewa leo Juni 4, 2026 na Kihongosi alipoenda kuzindua tawi hilo lenye wanachama zaidi ya 100, ikiwa ni sehemu ya zira yake aliyoanza leo mkoani Arusha akianzia Wilaya ya Karatu.

“Napongeza uhai wa chama kwenye hili shina ni wa asilimia 100, hivyo nitoe rai kwenu katika shina muendelee kutoa ada kama chama kinavyoelekeza”, amesema Kihongosi.

Pia, Kihongosi amewaahidi wakazi wa Kata ya Karatu, Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha kushughulikia suala la kuchonga barabara za mtaa, huku akiitaka TARURA kushughulikia suala hilo mapema iwezekanavyo.

Aidha Kihongosi, pia amezindua Shina la waendesha ‘Bodaboda’ Tawi la Karatu Mjini, huku akizitaka mamlaka husika kuwatengea eneo la kufanyia shughuli zao pamoja na kutoa mikopo ya asilimia 10 ili waweze kujikwamua kiuchumi.