June 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maofisa Habari watakiwa kuhabarisha taarifa sahihi

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

MAOFISA Mawasiliano wa Serikali,wanapaswa kuwahabarisha taarifa sahihi na kuwashirikisha wananchi ili waweze kujua na kutumia fursa za uwekezaji zilizopo kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali hapa nchini.

Hayo yameelezwa Juni 2,2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa,wakati wa mkutano mkuu wa mwaka 2026 wa Chama cha Maofisa Mawasiliano wa Serikali(TAGCO),unaofanyika jijini Mwanza kwa siku tano tangu Juni 1-5,2026,ambapo amesema taarifa sahihi zitasaidia wawekezaji wa ndani kufanya uwekezaji kupitia miradi hiyo ya maendeleo.

Huku akisisitiza umuhimu wa kutengeneza simulizi bora zinazoonesha mafanikio ya uwekezaji na utekelezaji wa mipango ya Serikali ili kuvutia fursa zaidi za maendeleo na uwekezaji nchini.

Msigwa amesema mawasiliano ya Serikali yanapaswa kubadilika na kwenda sambamba na mahitaji ya wakati kwa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu utekelezaji wa miradi na huduma zinazotolewa na Serikali.

“Tubadilike na tuoneshe kuwa tuna mchango katika taifa,tufanyie kazi changamoto tuwe na ubunifu na maarifa.Hivyo Maofisa Habari mnapaswa kutumia taaluma zenu kuandaa taarifa zenye tija ambazo zitasaidia jamii kuelewa na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na miradi ya maendeleo,”amesema Msigwa.

Sanjari na hayo Msigwa,amesema uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika miundombinu ya reli, barabara, nishati na kilimo ni miongoni mwa vichocheo muhimu vya ukuaji wa uchumi wa taifa,hivyo Maofisa Habari wanapaswa kuendelea kuelezea kwa kina maendeleo ya miundombinu hiyo inayotekelezwa hapa nchini ili wananchi waweze kuona matokeo ya uwekezaji unaofanywa katika sekta mbalimbali.

Aidha amewataka kuandika na kuripoti kwa kina kuhusu maboresho yanayofanyika katika sekta ya afya, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na hospitali katika maeneo mbalimbali hapa nchini,ili wananchi waweze kutambua juhudi zinazofanywa na Serikali.

Akifungua mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda,ameaema Mawasiliano ya Serikali si kazi ya kutuma taarifa kwa vyombo vya habari pekee,picha,mabango, matukio na taarifa za kawaida pekee bali ni sehemu ya uongozi, utekelezaji, uwajibikaji na kujenga imani ya umma.

“Taasisi inaweza kuwa na sera nzuri, mradi mkubwa, huduma muhimu au mageuzi ya msingi lakini kama wananchi hawaelewi,wadau hawapati taarifa sahihi,ujumbe unatoka kwa kuchelewa au kwa vipandevipande basi utekelezaji unaweza kudhoofika,”amesema Mtanda.