*Wamuomba Rais Samia kuingilia kati
Na Mwandishi Wetu,Tanga
Simanzi, vilio na hali ya sintofahamu vimetanda Kitongoji cha Bago, Kata ya Kigombe wilayani Muheza mkoani Tanga, baada ya wananchi wa kaya 67 kubaki bila makazi,wakidai nyumba zao kubomolewa na kampuni ya Amboni Plantation katika operesheni iliyotekelezwa Mei 22 mwaka huu.
Waathirika hao, ambao wengi wao ni familia za wafanyakazi wa zamani na vibarua wa mashamba ya mkonge, sasa wanaishi chini ya miti na katika mazingira magumu huku wakiiomba Serikali,Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati na kutafuta suluhisho la haraka la mgogoro huo ambao umeacha wanawake, watoto na wazee wakikabiliwa na maisha ya taharuki na kukosa huduma muhimu za msingi.

Uharibifu huo ulitokea katika Kijiji cha Msakangoto, ambapo Kampuni ya Amboni Plantation inayojihusisha na kilimo cha mkonge ilitekeleza amri ya mahakama ya kuwaondoa wakazi hao katika eneo hilo.
Hata hivyo, wananchi walioathirika wanadai kuwa utekelezaji wa amri hiyo ulifanyika katika mazingira yaliyojaa maswali mengi, huku baadhi yao wakieleza kuwa walikuta nyumba zao tayari zimebomolewa waliporejea kutoka mashambani.
Wakizungumza kwa uchungu wananchi hao wamesema mbali na kupoteza makazi yao, pia walipoteza mali mbalimbali ikiwemo fedha taslimu, mazao, samani na vifaa vya shule vya watoto wao, jambo ambalo limeongeza mateso kwa familia nyingi zilizokuwa tayari zikikabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Mmoja wa waathirika hao, Jane Sekela, amesema hali wanayoishi kwa sasa ni ya kusikitisha na imewafanya wajione kama wakimbizi ndani ya nchi yao wenyewe.
“Sisi ni watanzania lakini leo tunaishi kama wakimbizi.Mimi ni mama mwenye watoto nane sina mahali pa kuishi,mpaka sasa nalala nje,tumepoteza kila kitu tulichokuwa nacho. Tunamuomba Rais Samia asikie kilio chetu na atusaidie kwa sababu tumedhalilishwa na kunyanyaswa,”amesema kwa huzuni.
Kwa upande wake, Eva Stephen amesema, tukio hilo limeathiri kwa kiasi kikubwa ustawi wa watoto wake, hasa wale wanaojiandaa kufanya mitihani ya kitaifa.
“Niliporudi kutoka shambani nilikuta nyumba yangu imebomolewa. Kitu cha kwanza nilichokimbilia ni vifaa vya shule vya watoto wangu,nilifanikiwa kuokoa baadhi lakini niliporudi kuangalia vitu vingine nikakuta hakuna kilichobaki.Watoto wangu wameathirika kisaikolojia na hali hii imewavuruga sana wakati huu muhimu wa masomo yao,”amesema Stephen.

Naye Jane Francis,amesema familia nyingi sasa zinalala chini ya miti huku watoto wakishindwa kwenda shule kutokana na kupoteza madaftari na vifaa vya kujifunzia.
“Vifaa vya shule vimeharibika na vingine vimefukiwa kwenye vifusi. Hatujui kesho yetu itakuwaje tunaomba Serikali na Rais wetu watuangalie kwa jicho la huruma kwa sababu maisha yetu yamekuwa hatarini,” amesema Francis.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wameeleza kuwa hali hiyo ni ya kushtua na haikutarajiwa kutokea katika mazingira ya kawaida ya utekelezaji wa sheria.
Ally Mohamed,alisema tukio hilo limewaacha wengi wakiwa na maswali kuhusu namna operesheni hiyo ilivyotekelezwa.
“Tulikuwa tunaona matukio kama haya kwenye televisheni yakitokea nchi nyingine, lakini leo yametokea hapa kwetu. Hii ni hali inayoumiza na kuacha maswali mengi kuhusu haki na ustawi wa wananchi,”amesema.
Kufuatia hatua hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, ameunda kamati maalumu ya kuchunguza mazingira yote yaliyozunguka kutekeleza amri hiyo ya mahakama.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Dkt. Burian amesema kamati hiyo itafuatilia mchakato mzima wa utekelezaji wa amri hiyo, ikiwemo kubaini sababu za kutoshirikishwa kwa mamlaka husika katika operesheni hiyo pamoja na kujiridhisha kama maandalizi ya kuwapatia wananchi makazi mbadala na huduma muhimu yalifanyika kabla ya utekelezaji.
“Ni kweli kulikuwa na utekelezaji wa amri ya mahakama, lakini katika utekelezaji huo kuna masuala mbalimbali ambayo yanahitaji kufanyiwa tathmini. Tumeunda timu maalumu ili kufuatilia na kujiridhisha kuhusu hatua zote zilizochukuliwa katika mchakato huo,”amedema Dkt. Burian.
Amesema kamati hiyo itatoa mapendekezo yatakayosaidia kubaini ukweli wa tukio hilo na kuhakikisha haki inapatikana kwa pande zote zinazohusika.
Wakati uchunguzi huo ukiendelea, mamia ya wananchi walioathirika wanaendelea kuishi katika mazingira magumu wakisubiri majibu ya Serikali, huku wakitumaini kuwa sauti zao zitasikika na hatua stahiki kuchukuliwa ili kurejesha matumaini ya maisha yao.



More Stories
Dkt. afo awapambania Maafisa Maendeleo ya Jamii
Magu bingwa UMITASHUMTA
Mbarali yaweka mikakati thabiti kudhibiti mapato