June 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbarali yaweka mikakati thabiti kudhibiti mapato

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imesema imeweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa lengo la kudhibiti mianya ya upotevu unaosababishwa na baadhi ya watu wanaokwepa ushuru kupitia mbinu mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli, amesema kata zote 20 zimewekewa mageti ya ukusanyaji mapato, huku mfumo wa mageti ya dharura ukiwa umeanzishwa ili kukabiliana na matukio ya utoroshaji wa mazao na mapato.

“Kimsingi tuna mageti mengi katika kata zote, lakini tumeweka utaratibu wa kufungua mageti ya dharura pale tunapopata taarifa za utoroshaji wa mazao au changamoto nyingine. Hapo tunafungua geti na kuweka mkusanya ushuru kwa mujibu wa sheria ili kudhibiti upotevu wa mapato,” amesema Mweli.

Ameongeza kuwa halmashauri hiyo pia imegawa maeneo ya ukusanyaji mapato katika kanda tano, zikiwemo Madibila, Imalilo Songwe na Kapunga, kila moja ikiwa na wasimamizi maalum wanaofuatilia kwa karibu mwenendo wa makusanyo.

“Lengo ni kuwa na macho mengi zaidi katika usimamizi wa mapato. Kila kanda ina wasimamizi ambao wanahakikisha hakuna mianya ya upotevu wa mapato,” ameongeza.

Katika kuongeza ufanisi, Mweli amesema halmashauri hiyo inatumia vikosi kazi vya pamoja vinavyohusisha kamati ya usalama ya wilaya, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na watendaji wa kata kufanya doria za mara kwa mara na za kushtukiza.

Amesema doria hizo zimekuwa na mchango mkubwa kwani zimepunguza tabia ya baadhi ya watu kukwepa ushuru, huku wakilazimika kufuata taratibu za kisheria za ulipaji kodi na ushuru.

Aidha, amesema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na watendaji wa halmashauri wanaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini changamoto katika maeneo ya ukusanyaji mapato na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.

Kwa upande wake, mmoja wa wadau wa maendeleo, Nora Agustino, amesema hatua hizo zimeimarisha usimamizi wa mapato na kupunguza mianya ya upotevu iliyokuwepo awali.

Amesema kwa sasa kumekuwa na nidhamu kubwa katika ukusanyaji wa mapato kutokana na usimamizi thabiti wa uongozi wa halmashauri.

“Awali kulikuwa na watu wajanja waliokuwa wakikwepa mapato, lakini sasa tunaona uthibiti ni mkubwa zaidi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mweli amesema halmashauri hiyo inatarajia ongezeko la uzalishaji wa zao la mpunga kwa msimu wa kilimo 2025/2026, hali ambayo itaongeza mzunguko wa kiuchumi na mapato ya ndani.