


Na Mwandishi wetu,Dodoma
KATIKA kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora na ya gharama nafuu, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi, hususan vijana, kumudu kumiliki makazi.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Amina Lumuli, amesema kuwa TBA tayari imeanza kutekeleza miradi ya nyumba za gharama nafuu katika mkoa wa Dar es Salaam.
Lumuli ametaja Mradi wa Temeke Kota kuwa ni miongoni mwa miradi hiyo, akibainisha kuwa utekelezaji wa mpango huo utaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.
“Tunawakaribisha wawekezaji kuja kushirikiana nasi ili kwa pamoja tuweze kufanikisha lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 la kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora na ya gharama nafuu,” amesema Lumuli.
Aidha, Lumuli amesema utekelezaji wa mradi huu unatokana na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora na yenye gharama nafuu.
Amesema TBA itaendelea kuhakikisha makundi yote, yakiwemo makundi maalum, yanafikiwa na kunufaika na programu hii ya nyumba za gharama nafuu.

More Stories
TCAA yaimarisha dawati huduma kwa Wateja
Mtanzania Avith Philip ang’ara Orodha ya Wajasiriamali 100 Bora Afrika
Zanzibar yatumia Sabasaba kutangaza fursa za uwekezaji