May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe. (Picha na Mtandao)

Zitto apongeza nchi G20 kwa kusimamisha malipo ya madeni

Na Mwandishi Wetu

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amesema uamuzi wa nchi zenye Uchumi Mkubwa Duniani G20 kutoa nafuu ya madeni ni msaada mkubwa kwa mataifa yanayoendelea katika kipindi hiki cha mapambano ya ugonjwa wa Corona.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema;
“Nimepokea kwa furaha uamuzi wa nchi zenye Uchumi Mkubwa Duniani, G20 wa kusimamisha malipo ya madeni ya nchi zinazoendelea ili ziweze kupambana na janga la Corona.”

Uamuzi huo uliofikiwa juzi, Aprili 15, Aprili mwaka hii na kusisitiza kwamba; “Ni uamuzi wa kihistoria na unaojali maslahi mapana ya Dunia.

Nawashukuru sana Viongozi wote wa Mataifa ya G20 kwa maamuzi haya.”

Zitto alipotoa hotuba yake kupitia mitandao ya kijamii Aprili 3, mwaka huu aliwaeleza Watanzania kuwa wanafanya juhudi ili mataifa yaliyoendelea yakubali kusimamisha malipo ya madeni kwa mwaka mmoja.

Alisema Tanzania inatumia takribani sh. trilioni 4 kila mwaka kuhudumia deni la nje. Katika taarifa iliyotolewa juzi mataifa ya G20 yalitoa nafuu hiyo kuanzia Mei 1, mwaka huu hadi mwisho wa mwaka 2020.

Zitto alisema hilo ni jambo la kushukuru sana kwani si haba, na uamuzi huo utasaidia sana kukabiliana na athari za janga la corona.

Hata hivyo, alitoa wito kwa Benki ya Dunia na IMF kama waratibu wa nafuu hiyo ya madeni kuhakikisha kuwa nchi husika zinakuwa na mpango madhubuti wa kuigeuza nafuu hiyo kuwa fursa ya maendeleo ya watu.

” Vile vile nchi zitakazo faidika na nafuu hii lazima kwanza kuonesha mpango unaotekelezeka wa kuimarisha sekta ya afya kwa upana wake ikiwemo maji safi na salama na pia kuwepo kwa mfumo
wa uwajibikaji ili kuzuia matumizi mabaya na ubadhirifu wa Fedha hizi,” alisema Zitto.

Alisema ACT Wazalendo kama chama pekee kilichoongoza juhudi za
kupata nafuu hii nchini na wataendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa fedha hizi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.