May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya 1000 kushiriki kongamano la 32 la kitaifa la wahandisi

Na Mwandishi wetu Timesmajira online

TAASISI ya Wahandisi Tanzania (IET) imesema zaidi ya washiriki 1000 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano la 32 la Kitaifa (National Conference) la wahandisi Novemba 30 hadi Desemba 2 mwaka huu katika ukumbi wa kimataifa Arusha (AICC) jiijini Arusha.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es salaam Novemba 23, 2023 na Rais wa IET Mhandisi Dkt. Gemma Modu wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Mhandisi Dkt. Modu amesema kongamano hilo wanaliandaa kwa kushirikiana na Bodi ya Usaili wa Wahandisi (ERB) na Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania (ACET).

Amesema kongamano hilo litajumuisha wahandisi, mafundi wanafunzi na wadau wengine kutoka mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi.

“Kongamano hili muhimu na kuna baadhi ambao watashiriki kwa njia ya mtandao,tunakadiria kuwa na washiriki zaidi ya 1000,”amesema Dkt. Modu.

Dkt Modu amesema katika kongamano hilo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.

Dkt Modu ameeleza kuwa dhima ya mkutano huo ni “Innovative Solutions in Engineering for Sustainable Development” ambapo kwa tafsiri ni (Suluhisho za Ubunifu katika Uhandisi kwa Maendeleo Endelevu).

Vilevile amesema lengo ni kuweza kuendana na kukidhi matakwa ya maendeleo ya teknolojia na kuweza kusaidia nchi kutatua changamoto katika sekta mbalimbali za kiuchumi, pia kutoa suluhusho la matatizo katika jamii.

Aidha amewaomba Wahandisi na wadau wote wa sekta mbalimbali za uchumi nchini kushiriki kwenye kongamano hilo muhimu.

Naye Mjumbe wa Baraza la Utendaji wa IET Mhandisi Pendo Haule amewaomba na kuhimiza kampuni za wazawa kujitokeza kuchukua miradi pindi inapotangazwa ili kuonesha ujuzi na utaalam wao.