Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas inayomilikiwa na AXIAN Telecom, imeendelea kupata mafanikio makubwa baada ya kutajwa kama moja ya chapa za kufuatiliwa barani Afrika kupitia ripoti ya Brand Finance Africa 200, 2026.
Pia, imeingia kwa mara ya kwanza kwenye orodha hiyo ikiwa na thamani ya chapa ya dola za Marekani milioni 277.
Yas imeshika nafasi ya 61 kwa ujumla na nafasi ya 43 kwa ubora wa nguvu ya chapa, ikiwa na alama 84.8 kati ya 100.
Utambuzi huo unaongeza hatua nyingine muhimu katika safari ya Yas kujijenga kama moja ya simulizi kubwa za mafanikio ya mabadiliko ya chapa barani Afrika, baada ya pia kutambuliwa kimataifa mapema mwaka huu kupitia ripoti ya Brand Finance Telecoms 150, 2026.
Kuingia kwa Yas katika orodha ya Brand Finance Africa 200, 2026 kunaonyesha namna chapa hiyo inavyoendelea kupata nguvu na ushawishi katika bara zima la Afrika, sambamba na uwekezaji wake unaoendelea katika upanuzi wa mtandao.
Akizungumzia mafanikio hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa AXIAN Telecom, Hassan Jaber amesema kutambuliwa na Brand Finance Africa 200 pamoja na chapa kubwa barani Afrika ni ishara kuwa mkakati wa kampuni hiyo unaendelea kuzaa matunda.
“Katika kipindi cha mwaka mmoja tu, Yas imekua kutoka kwenye chapa mpya sokoni na kuwa chapa inayowagusa wateja moja kwa moja katika masoko yetu mbalimbali na kujijengea heshima katika bara zima la Afrika.
Utambuzi huu unazidi kuimarisha dhamira yetu ya kuwa mshirika wa kuaminika wa kidijitali barani Afrika, pamoja na kuendelea kuwekeza katika miundombinu, ubunifu na uzoefu unaofanya maono hayo kuwa halis,” amesema.
Akizungumzia mafanikio hayo, Oliver Schmitz, Mkurugenzi Mkuu wa Brand Fiannce Africa, amesema mabadiliko ya chapa ya AXIAN Telecom kwenda Yas ni miongoni mwa kampeni zilizofanikiwa zaidi za kubadili chapa kwa kiwango kikubwa kuwahi kushuhudiwa barani Afrika.
Ameeleza kuwa kilichovutia zaidi si tu kuundwa kwa chapa mpya ya panafrika, bali namna AXIAN Telecom ilivyoweza kuhamisha thamani, imani na ushawishi wa chapa zake za zamani kwenda Yas bila kupoteza uaminifu wala umuhimu wake kwa wateja.
Kwa mujibu wa utafiti wa Brand Finance, AXIAN Telecom imefanikiwa kuendeleza sifa muhimu za chapa zake za awali – ikiwemo kuaminika, kutoa thamani na kuendelea kuwa karibu na mahitaji ya soko – huku ikiijenga Yas kama chapa yenye mtazamo wa baadaye na uwezo wa kushindana kikanda.
Mafanikio hayo yanaonekana kupitia kuingia kwa nguvu kwa Yas katika orodha ya Telecoms 150 pamoja na kutambuliwa kwake kwenye viwango vya Africa 200 2026, ambapo sasa inatajwa kuwa moja ya simulizi kubwa za mafanikio ya mabadiliko ya chapa barani Afrika.
Schmitz ameongeza kuwa Yas inaonyesha wazi kuwa mchakato wa kubadili chapa unapojengwa katika mkakati madhubuti, utekelezaji makini na uelewa wa mahitaji ya wateja, unaweza kuongeza thamani ya chapa pamoja na kuimarisha ushindani katika soko la kidijitali la Afrika linalokua kwa kasi.

More Stories
Mke adaiwa kumuua Mumewe kwa sindano yenye sumu
Mke adaiwa jumuia Mumewe kwa sindano yenye sumu
Takukuru yageukia utapeli kwenye makundi ya WhatsApp