March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya wajumbe walioshiriki mkutano wa uzinduzi wa mpango huo.

Wizara ya Fedha na Mipango yazindua Mpango wa Maendeleo Sekta ya Fedha

Na Joyce Kasiki,timesmajira online,Dodoma

WIZARA ya Fedha na Mipango imezindua Mpango wa Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia 2019/2020 hadi 2029/2030 ambao pamoja na mambo mengine umelenga kudhibiti utakatishaji fedha haramu.

Mpango huo pia umelenga kuongeza wigo na fursa za upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi wote zikiwemo za bima.

Akizindua mpango huo jana jijini hapa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dotto James, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mary Maganga, amesema mpango huo utaongeza wigo katika upatikanaji wa huduma za mikopo, akiba, uwekezaji na kuongeza mchango wa sekta ya fedha katika ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na sekta ya viwanda.

Amesema mpango huo umeandaliwa ili utumike kama nyenzo ya kutatua changamoto zilizopo ambapo pamoja na mambo pia umelenga kuongeza upatikanaji mitaji ya muda mrefu, upatikanaji huduma jumuishi za fedha na kulinda watumiaji wa huduma za fedha.

Pia utaimarisha uthabiti wa sekta ya fedha ,kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya fedha na kuweka mazingira wezeshi ya sheria ,kanuni ,taratibu na miongozo katika sekta ya fedha.

Amewataka wadau wa sekta ya fedha ndani na nje ya Serikali kutambua kuwa uzinduzi wa mpango huo ni mwanzo wa mambo mengine yanayotakiwa kufanyika katika sekta ya fedha kwa kuleta mageuzi makubwa na maendeleo katika kipindi cha miaka kumi ijayo.

Aidha amewataka waratibu na wasimamizi wa mpango huo kuwianisha mipango mbalimbali ili iendene na mpango huo Mkuu wa Kitaifa katika maeneo wanayoyasimamia .

“Maeneo hayo ni katika sekta ndogo zilizomo ndani ya sekta hii ikiwa ni pamoja na benki, bima, masoko ya mitaji na dhamana, mifuko ya hifadhi ya jamii na sekta ya huduma ndogo za fedha.”amesema Maganga.

Kwa upande wa vyuo vikuu na taasisi za utafiti, amewataka kuona fursa zilizopo katika mpango huo na kujipanga kuboresha maeneo mbalimbali ya kitaaluma na ya kiutafiti ili kuhakikisa sekta hiyo inaendelea kuwa yenye ushindani na kuweza kuhimili mabadiliko ya nyakati kwa wepesi na weledi.

Akitoa maelezo ya mpango huo, Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja, amesema wakati wa maandalizi,timu ya wataalam wa mpango huo ilifanya mapitio kwenye nyaraka mbalimbali zikiwemo taarifa za maboresho ya sekta ya fedha, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, Dira ya Taifa ya Maendeleo Zanzibar ya mwaka 2020 na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (ZSGRP III).

Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, akitoa maelezo ya utangulizi kuhusu Mipango huo

Pia ilipitia Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano 2016/17-2020/21 na taarifa ya Programu ya Tathimini ya Sekta ya Fedha ya mwaka 2018 kwa lengo la kupata matokeo zaidi katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Kitaifa.