Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WIZARA ya Afya imesema hadi sasa Tanzania haina mgonjwa wala ugonjwa wa ebola na hali ya usalama wa afya nchini iko vizuri.Huku ikitaka wananchi waendelee kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya.
Imesema kutokana na mwingiliano wa watu na shughuli za kijamii na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi jirani, Serikali imeendelea kuchukua hatua za mapema na za kina ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini na imejipanga kikamilifu kuzuia, kugundua mapema na kudhibiti tishio lolote la kuhatarisha afya ya watanzania wote kupitia mifumo yake ya kitaifa ya ufuatiliaji, utambuzi na udhibiti.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Juni 18,2026 na Waziri wa Wizara hiyo Mohamed Mchengerwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa tishio la ugonjwa wa ebola na hatua zinazoendelea kuchukuliwa ili kuzuia na kuimarisha utayari.
“Mtakumbukwa kuwa, mnamo tarehe 15 Mei, 2026 nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda zilitoa taarifa ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini humo, na Shirika la Afya Duniani likatangaza kuwa ni dharura ya kiafya ya kimataifa. Aidha, tarehe 18 Mei, 2026, Serikali kupitia Mganga Mkuu wa Serikali ilitoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu tahadhari dhidi ya tishio la ugonjwa huo na hatua za kuchukua. Hadi sasa, ugonjwa huo umeendelea kuenea na kuathiri jamii katika nchi hizo; hivyo, wito unaendelea kutolewa wa kuimarisha afua za udhibiti na kuzuia usisambae na kuingia katika nchi zingine ikiwemo Tanzania,”amesema Mchengerwa.
Amesema kufuatia tishio hilo, Wizara ilitoa Mwongozo wa Wasafiri (Travel Advisory) Na. 17 wa tarehe 19 Mei 2026 kwa wasafiri wote wanaoingia nchini, ukiainisha hatua za kinga na udhibiti zinazopaswa kutekelezwa na wasafiri kwa mujibu wa Kanuni za Afya za Kimataifa na Sheria ya Afya ya Jamii ili kuzuia kuingia kwa maambukizi nchini na kudhibiti uwezekano wa kusambaa kwa ugonjwa.
Pamoja na hayo Mchengerwa amesema Serikali imeendelea kuchukua na kuimarisha ufuatiliaji wa tetesi katika jamii na uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia nchini kupitia mipaka, bandari na viwanja vya ndege ili kubaini mapema viashiria vya ugonjwa.
“Mpaka sasa, jumla ya tetesi 64 kutoka Mikoa 21 zimeripotiwa, kati ya hizo wahisiwa 11 walikidhi vigezo, wakachukuliwa sampuli na baada ya kupimwa wakathibitika hawana maambukizi ya Ebola,”amesema.
Aidha amesema serikali imeimarisha utayari wa wataalam wa kitaifa na vituo vya huduma kote nchini pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa kinga na tiba muhimu ili kutoa huduma kwa wagonjwa endapo ugonjwa utaingia nchini, sambamba na kusambaza miongozo na vitendea kazi kwa mikoa ili kusaidia wataalam walioko mstari wa mbele kujikinga ipasavyo na kutoa huduma bora endapo itahitajika.
Pia amesema Serikali imehakikisha upatikanaji wa vifaa kinga maalumu, vifaa tiba na vifaa vingine muhimu kwa watoa huduma wa afya waliopo mstari wa mbele. Hadi sasa, seti za kutosha za vifaa kinga hivyo vipo katika Bohari ya Dawa (MSD) na mikoa yote kwa ajili ya matumizi ya dharura. Hatua hii inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha hakuna mhudumu wa afya anapata maambukizi au kupoteza maisha akiwa katika jukumu la kuokoa maisha ya wengine. Kwa msingi huo, hatua zote muhimu zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama, ustawi na ulinzi wa wataalam wa afya wakati wote.
Pamoja na hayo Mchengerwa amesema mafanikio ya kuilinda nchi dhidi ya Ebola hayategemei Serikali pekee. Yanahitaji ushirikiano wa kila mwananchi, viongozi wa jamii, Taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wote wa maendeleo.
“Nawaombeni tuendelee kushirikiana na kufuata maelekezo ya wataalam wa afya, kutoa taarifa mapema za wahisiwa na kupuuza taarifa za upotoshaji zinazoweza kuleta hofu au taharuki isiyo ya lazima. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kushiriki katika kuilinda Tanzania dhidi ya tishio hili,”amesema.

More Stories
Mwenge wa Uhuru wawasili Mkoani Tanga
BRELA yatoa elimu wiki Utumishi wa Umma
SELF yatangaza fursa lukuki maonesho wiki Utumishi wa Umma