Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOline,Zanzibar
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeahidi kutekeleza ushauri uliotolewa na Benki ya Dunia katika utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania (PAMOJA), unaotekelezwa kwa kushirikiana na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA).
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abeida Rashid Abdallah, baada ya kumalizika kwa kikao kifupi kati ya wizara hiyo na ujumbe kutoka Benki ya Dunia, kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika ofisi za wizara, Kinazini, Unguja.
Amesema kikao hicho kimetoa nafasi ya kubadilishana mawazo na ushauri kuhusu utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2024 hadi 2029.

Abeida amesema wizara imepokea ushauri mbalimbali uliotolewa na Benki ya Dunia, ikiwemo umuhimu wa kushirikisha jamii kwa karibu ili kuongeza uelewa kuhusu mradi huo pamoja na kuongeza kasi ya utekelezaji wake.
Ameeleza kuwa Benki ya Dunia imetoa zaidi ya sh.bilioni 33 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa PAMOJA, wenye lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kupunguza vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.
“Lengo la ujio wa ujumbe huo ni kuona hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi pamoja na kushauriana kuhusu njia bora za kuendeleza mradi huo,”amesema Abeida.

Aidha,amesema kupitia mazungumzo yao wamekubaliana kuongeza ushirikishwaji wa jamii katika ngazi za chini ili wananchi wapate uelewa wa namna mradi huo utakavyowanufaisha wanawake kupitia fursa za mikopo pamoja na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Mradi huu utawainua kiuchumi vijana na wanawake wenye sifa zitakazowawezesha kupata mikopo. Pia tutajenga nyumba salama mbili, moja Unguja na nyingine Pemba, kwa ajili ya kuhifadhi wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhani Mohd, amesema mradi huo hautawanufaisha wanawake pekee bali pia wanaume watanufaika kupitia uwezeshaji wa kiuchumi utakaosaidia kujenga jamii yenye mtazamo mpana wa maendeleo.

Amesema anaamini Mradi wa PAMOJA utaleta mabadiliko makubwa kwa wananchi kwa kuwa umejikita katika kuwawezesha wanawake kiuchumi na kupambana na vitendo vya udhalilishaji katika jamii.
Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Uendelevu wa Kijamii na Ujumuishi kutoka Benki ya Dunia, Valarakshmi Vemuru, amesema mradi huo unalenga kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake pamoja na kuwasaidia kujinusuru dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Amesema pia mradi huo unazingatia malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto (ECD) ili kuwapa wanawake nafasi nzuri ya kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Vemuru aliitaka Wizara kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unatoa matokeo chanya kwa wananchi, huku akisisitiza matumizi sahihi ya fedha zilizotengwa kwa utekelezaji wake.

Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania (PAMOJA) ni mradi wa miaka mitano unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na ZEEA, ukiwa na lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi na kupambana na vitendo vya udhalilishaji katika jamii.


More Stories
Aga Khan Hospital yaja na suluhisho ya changamoto ya Uzito uliopitiliza
Ruth Zaipuna kuipeleka NMB Jukwaa la Kimataifa Cambridge
TPDC yaongoza uchimbaji wa Gesi Songo Songo