May 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WFP laipatia serikali ndege nyuki,vishkwambi 370

Na Prona Mumwi

Waziri wa Kilimo,Hussein Bashe amepokea vifaa vya kisasa vya kilimo vya ndege nyuki (drone) na vishkwambi 370 kutoka Shirika la Chakula Duniani (WFP) leo tarehe 28 Agosti 2023, jijini Dodoma.Waziri Bashe amesema kuwa vifaa hivyo vitasaidia kukabiliana na visumbufu vya mazao shambani ili kilimo kiwe na tija katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema drone hiyo kubwa yenye uwezo wa kupulizia dawa na viuatilifu katika hekta 20 na vishkwambi 370 vyenye thamani ya shilingi milioni 364 vitarahisisha utekelezaji wa dhana ya kilimo ni sayansi kwa kuwa vitatatua changamoto za Wakulima.

“Nawashukuru sana WFP kwa kutupatia vifaa hivi, ambapo vishkwambi vinakwenda kugawiwa kwa Maafisa Ugani kwa ajili ya kukusanya taarifa mbalimbali za Kilimo,” amesema Waziri Bashe

Waziri Bashe ameeleza kuwa vifaa vya drones na vishkwambi 370 vitaanza kutumika kwa kupima mashamba ya vijana wa programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Build a Better Tomorrow – BBT) ili kuona kama yana visumbufu vya mazao ili waweze kuvidhibiti kabla hawajaanza kulima.

“Ushirikiano huu na Shirika la Chakula Duniani (WFP) wa kupatiwa vifaa unaoonesha jinsi gani wadau wanavyounga mkono jitihada za Serikali katika kukuza kilimo hapa nchini,” amesema Waziri Bashe.

Waziri Bashe amesema kuwa Serikali imepanga kuanzisha kituo kimoja kwa ajili usimamizi wa drones hizo ikiwemo kufuatilia taarifa za visumbufu vya mazao.

Naye Mwakilishi Mkazi wa WFP, Sarah Gibson amesema kuwa amefurahishwa na ushirikiano aliopewa na Wizara huku akiahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali ili kuhakikisha wanakuza na kuendeleza shughuli za Kilimo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea (TPHA), Profesa Joseph Ndunguru amesema kuwa vifaa hivyo vimekuja wakati muafaka ili kuleta Kilimo chenye tija.