May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shinyanga yatakiwa kuoengeza kasi ukusanyaji mapato

Na Suleiman Abeid
Timesmajira Online, Shinyanga

HALMASHAURI ya wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga imetakiwa kuongeza kasi katika ukusanyaji wa mapato yake ya ndani ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Halmashauri hiyo ikiwemo kulipa deni la zaidi ya shilingi milioni 900.

Agizo hilo limetolewa na Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga, Saidi Kitinga wakati akitoa maelekezo ya Serikali kwenye mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambao pamoja na mambo mengine ulipitisha taarifa ya hesabu za mwisho kwa mwaka 2022/2023.

Kitinga amesema pamoja na kwamba Halmashauri hiyo inakwenda vizuri hivi sasa katika utekelezaji wa shughuli zake lakini kasi ndogo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani inaweza kuchangia kukwama kukamilika kwa wakati kwa miradi mingi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wake.

“Niseme jambo moja muhimu, ndugu zangu ni lazima tupambane katika suala zima la ukusanyaji wa mapato, na kwa msingi huo vyanzo vyetu vyote vya mapato lazima vifahamike, tumeona hapa tuna madeni zaidi ya shilingi milioni 900 mnadaiwa, haya madeni yatalipika tu iwapo mtakuwa na mapato ya kutosha,”

“Ikiwezekana tuwe na vikao vya kila mwezi kuangalia jinsi gani shughuli za ukusanyaji wa mapato zimefanyika, lakini tutengeneze pia kikosi kazi kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato, mheshimiwa Rais anatoa fedha nyingi kwa ajili ya shughuli za maendeleo, lakini tusipokusanya fedha za kutosha, tunaweza pia kuzikosa fedha hizo,” ameeleza Kitinga.

Amesema ushirikiano kati ya watendaji, madiwani na maofisa watendaji katika kila kata ni wa muhimu kwenye suala zima la ukusanyaji wa mapato ya ndani badala ya kuwaachia watu wa idara ya mapato peke yao na pia elimu juu ya umuhimu wa kulipa ushuru na kodi mbalimbali za Halmashauri itolewe kwa wananchi.

Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmedi Salumu ametoa ushauri wake kwa wataalamu wa Halmashauri hiyo wawe na utaratibu wa kuhakikisha kila mradi unaohusu majengo mbalimbali yanayojengwa uwekewe bajeti kamilifu badala ya kutenga fedha nusunusu.

“Tunapopeleka fedha kwenye ujenzi wowote ule, mfano pale Zahanati ya Songambele, basi tuhakikishe tunapeleka fedha za kukamilisha kazi yote na jengo lianze kutoa huduma badala ya kupanga kidogo kidogo, na mwaka unaofuata hatulipangii tena bajeti, hivyo ujenzi unasimama,”

“Sasa tumefanya tathimini gani ya majengo haya ambayo tumeyapangia fedha halafu mwaka unaokuja hatuweki fedha, kisha mwaka mwingine unaokuja tunaweka fedha, hili tulifanyie kazi, tufanye tathimini ya majengo yote ambayo hayajakamilika ili tuyawekee bajeti kamili na yakamilishwe ujenzi wake, badala ya kutenga kidogo kidogo,”amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Ngassa Mboje amesema moja ya mikakati ya Halmashauri yake kwa mwaka huu wa fedha ni kuhakikisha wanaongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuweza kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imepangwa kutekelezwa.

“Tumejipanga vizuri katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya ndani na tunaamini tutafanikiwa, Halmashauri tunadaiwa zaidi ya shilingi milioni 900, lakini na sisi tunadai shilingi milioni 593, sasa tutasimama kidete kuhakikisha tunalipa madeni yote tunayodaiwa kwa kuzingatia bajeti yetu, na wale tunaowadai tunaomba watulipe,”ameeleza Mboje.

Katika taarifa yake kwa madiwani Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, David Lwazo amesema pamoja na kukamilisha ufungaji wa hesabu za Halmashauri kwa wakati lakini hadi kufikia Juni 2023 halmashauri ilikuwa ikidaiwa kiasi cha shilingi 945,738,589.88 huku ikidai shilingi 593,630,147.00.

“Mheshimiwa mwenyekiti naomba niahidi katika kikao chako hiki kwamba, tutatekeleza maelekezo yote ambayo yametolewa hapa, na pia mmeagiza tuwe na kikosi kazi kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato yetu hilo tutalitekeleza na tayari tumeanza na vilevile tutahakikisha tunakuwa na matumizi sahihi ya fedha wakati wote,” ameeleza Lwazo.