May 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ndejembi,Dkt.Ramokgopa wakubaliana kuimarisha Ushirikiano wa Nishati

📌 Tanzania yaweka wazi mpango wa kuanza kuzalisha umeme kwa makaa ya mawe.

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Waziri wa Nishati wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amefanya mazungumzo na Waziri wa Umeme na Nishati wa Afrika Kusini, Dkt. Kgosientsho Ramokgopa, mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika wanaoshughulikia sekta za Nishati na Uchukuzi.

Katika mazungumzo hayo, Ndejembi ameeleza kuwa Tanzania ina mpango wa kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe yanayopatikana nchini, sambamba na kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia nishati ya upepo ili kupanua wigo wa vyanzo vya umeme na kuimarisha uhakika wa nishati.

Kwa upande wake, Afrika Kusini imeendelea kuwa kinara katika uzalishaji wa umeme barani Afrika, ikiwa na uwezo wa takribani megawati 63,000 (≈ 63 GW), kati ya kiwango hicho, takribani asilimia 70 ya umeme huzalishwa kupitia makaa ya mawe sawa na MW 45,000, huku nishati ya upepo ikichangia takribani asilimia 5 sawa na MW 3,000 hatua inayoonesha uzoefu mkubwa wa nchi hiyo katika matumizi ya vyanzo mbalimbali vya nishati.

Kutokana na uzoefu huo, Mawaziri hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya nishati, hususan katika uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo mseto, pamoja na kubadilishana uzoefu na utaalamu ili kuongeza ufanisi wa sekta hiyo katika nchi zao.

Aidha, wamekubaliana kuendeleza ushirikiano wa taasisi kupitia Eskom (Shirika la Umeme la Afrika Kusini), shirika kubwa la umeme barani Afrika, kushirikiana na TANESCO (Shirika la Umeme Tanzania) pamoja na REA (Wakala wa Nishati Vijijini). Ushirikiano huo utalenga kuwajengea uwezo wataalamu wa Tanzania katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, kwa lengo la kuimarisha zaidi sekta ya nishati nchini.

Katika kuendelea kuimarisha ushirikiano huo, Dkt. Ramokgopa ameahidi kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania, ambapo ameweka wazi kuwa ataambatana na wataalamu kutoka sekta ya nishati ili kujionea fursa zilizopo pamoja na kubadilishana uzoefu na wenzao wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya umeme.