May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu wa Ethiopia ziarani nchini kesho, kuteta na Rais Samia

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Dkt. Abiy Ahmed Ali anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia kesho hadi Machi 2 Machi, 2024 kwa mwaliko wa Raais Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Abiy atapokelewa rasmi Ikulu, Dar es Salaam Machi 1, 2024 na mwenyeji wake Rais Samia.

Akiongelea ziara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba,, alisema lengo la ziara hii mbali na kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili, inalenga pia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ethiopia ambazo zimekuwa zikishirikiana katika maeneo ya biashara na uwekezaji, elimu, utamaduni, usafirishaji wa anga, kilimo, mifugo, udhibiti wa uhamiaji holela, ulinzi na usalama.

“Tanzania na Ethiopia zina uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu na wa kihistoria ambao ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mtawala wa Ethiopia, Hayati Haile Selassie. Viongozi hawa walishirikiana bega kwa bega katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na ni miongoni mwa Viongozi Waanzilishi 32 wa Umoja wa Afrika wakati huo OAU mwaka 1963,” amesema Waziri Makamba.

Waziri Makamba ameongeza kuwa, mbali na ushirikiano wa kidiplomasia, Tanzania na Ethiopia zinashirikiana katika sekta ya anga ambapo mwaka 2016 hadi 2023 jumla ya marubani 75 na wahandisi 25 kutoka Tanzania wamepokea mafunzo katika ngazi tofauti nchini Ethiopia. Hivyo ni wazi kuwa, ziara hii itafungua milango zaidi ya ushirikiano kati ya Shirika la Ndege la Ethiopia na Shirika la Ndege la Tanzania – ATCL katika kujiendesha kibiashara.

Hali kadhalika, Tanzania na Ethiopia zinashirikiana katika sekta ya mifugo na kilimo. Nchi hizi zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo kama kahawa, chai, asali, mbogamboga na matunda barani Afrika. Kupitia ziara hii Tanzania na Ethiopia zitaimarisha ushirikiano katika masuala ya umwagiliaji, matumizi ya teknolojia katika kilimo na matumizi ya mbegu zenye ubora na uhakika wa mavuno sambamba na tafiti katika sekta hizo mbili.

“Kuhusu sekta ya nishati, ziara hii itaziwezesha Tanzania na Ethiopia kujengeana uwezo na kubalishana uzoefu katika uzalishaji wa umeme unaotosheleza mahitaji ya nchi pamoja na kuzalisha umeme wa kibiashara utakaoiwezesha Tanzania kuuza katika nchi mbalimbali kupitia uanachama wake katika Jumuiya ya kuuziana umeme ya Afrika Mashariki (East African Power Pool), amesema Waziri Makamba.

Aidha, katika sekta ya elimu ziara hii itaziwezesha nchi hizi mbili kubadilishana wanafunzi na kujenga uwezo katika uuandaji wa mitaala na Tanzania kupata fursa ya kufundisha Kiswahili nchini Ethiopia.

Waziri Mkuu Abiy na ujumbe wake wataondoka nchini kurejea Ethiopia Machi 2, 2024.