April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu aweka jiwe la msingi ujenzi wa majengo CBE Mbeya

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi zote zinazokusanya mapato nchini zihakikishe zinaweka mipango endelevu itakayoziwezesha kusimamia matumizi ya mapato hayo kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kusimamia taasisi zote zinakusanya mapato na kuweka mifumo imara ya kusimamia matumizi yake.

Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Novemba 30, 2021) baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Mbeya. Mradi huo unajengwa katika kata ya Iganzo jijini Mbeya unagharimu sh. milioni 852.

Pia, Majaliwa amesema kuwa Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha inaweka mipango madhubuti na usimamizi sahihi wa biashara na wafanyabiashara ili waweze kunufaika zaidi na shughuli wanazozifanya.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa uongozi wa chuo cha CBE uendelee kuweka mipango ya kuwafikia wanyabiashara wa ngazi zote na hata wale ambao hawajaanza kufanya biashara ili waweze kuwatoa uoga wa uanzishaji wa biashara.

“CBE endeleeni kuweka mpango mzuri wa kuwafikia na kuwapa elimu ya biashara wafanyabiashara wakubwa, wakati na wadogo ili kuwawezesha kufahamu namna bora ya kuzifanya biashara zikue zaidi na kuongeza tija.”

Amesema katika kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi, Serikali iliwaagiza viongozi wa Serikali za Mitaa kwa kushirikiana nao watafute maeneo mazuri na kuyawekea miundombinu muhimu.

Naye, Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Emmanuel Mjema amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Juni mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu, ambapo chuo hicho kimetoa sh. milioni 502 na Serikali Kuu imetoa sh. milioni 350 kwa ajili ya ujenzi huo.

Amesema Chuo cha CBE kampasi ya Mbeya kilianza mwaka 2013 kikiwa na wanafunzi 44 na sasa kina wanafunzi 947. Ongezeko hilo linaonesha kuwa chuo hicho kinaendelea kuaminika zaidi katika utoaji wa elimu ya biashara na ujasiriamali nchini.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amefungua kiwanda cha Raphael Group cha kuongeza thamani zao la mpunga na mazao mengine kilichopo katika eneo la Uyole jijini Mbeya na kumpongeza mwekezaji huyo kwa hatua hiyo.

“Nampongeza Mkurugenzi wa kiwanda hiki Bw. Raphael Ndelwa kwa kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Samia za kuhamasisha uwekezaji sambamba na ujenzi wa viwanda ili kuwezesha bidhaa mbalimbali kuzalishwa nchini.”

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa taasisi za Serikali zinazojihusisha na sekta ya uwekezaji kutowasumbua wawekezaji bali wawaelimishe na kuwasaidia ili waweze kukuza zaidi shughuli zao. “Wawekezaji hawa wanaweka pesa nyingi sana kwenye eneo hilo, ni lazima tuwaunge mkono.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda hicho Ndelwa amesema kampuni yao inafanyakazi kwa mfumo wa kilimo cha mkataba na wakulima zaidi ya 14,000 ambao kati yao 7,800 wamejiajiri katika kilimo cha mpunga na 5,800 wanalima maharage.