Na Mathias Canal,Simiyu
KULINGANA na kuchelewa kuanza kwa maadhimisho ya wakulima (Nanenane) Mwaka 2020 katika baadhi ya Kanda kutokana na ugonjwa wa homa ya Mapafu (Corona) serikali imetangaza kuongeza siku mbili za maadhimisho ya sherehe hizo.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea Banda la Chama Cha Wanawake wafanyabiashara Tanzania (TABWA) kwenye viwanja vya Maonesho ya wakulima (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Amesema kuwa kulingana na mahitaji ya sherehe za wakulima kujifunza mbinu bora za kilimo wananchi ambao hawakupata fursa awali watatumia nafasi hiyo kujionea mbinu bora za kilimo, mifugo na uvuvi.
Amesema kuwa malengo makubwa ya sherehe hizo ni pamoja na kuwaunganisha wakulima, wafugaji, wavuvi na wanaushirika kusherehekea kwa pamoja ikiwa ni pamoja na kuonesha teknolojia ya zana bora za kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Kadhalika Waziri Hasunga amesema kuwa maonesho hayo yanatoa fursa ya kuwakutanisha wakulima, wavuvi na wafugaji na watoa huduma za fedha, bima, mawasiliano, taasisi za umma na binafsi.
Maonesho ya sherehe hizo yanafanyika katika kanda mbalimbali ikiwemo kanda ya Mwanza, Tabora, Simiyu, Mbeya, Dodoma, Morogoro, Arusha na Lindi
Katika maonesho hayo wakulima, wafugaji na wavuvi wanahamasishwa kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambapo wametakiwa kuchagua viongozi bora wenye uwezo wa kuendeleza kilimo.
“Maonesho hayo yanachagizwa na Kauli mbiu isemayo “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Chagua Viongozi Bora 2020” hivyo Wakulima, wafugaji na wavuvi nchini wapo tayari kwa Uchaguzi Mkuu na kutokana na mafanikio ambayo serikali ya Awamu ya Tano imepata katika sekta hizi, watakipatia Chama cha Mapinduzi ushindi mnono” amesisitiza Waziri Hasunga
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba