March 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wauguzi na wakunga wasiohusisha leseni zao kuchukuliwa hatua

Na Catherine Sungura-WAMJW,Dodoma

WAUGUZI na Wakunga ambao watakuwa hawajahuhisha leseni zao ndani ya miezi sita kuchukuliwa hatua, ikiwemo kufutwa kwenye daftari la Uuguzi na Ukunga, hivyo kutoruhusiwa kutoa huduma kwenye vituo vya afya vya umma au binafsi.

Wakuu wa wauguzi wakifuatilia uwasilishaji wa mada ikiwa ni siku ya pili ya kikao kazi kinachowakutanisha viongozi hao kutoka wilaya kumi na mbili nchini.Picha na Catherine Sungura

Hayo yamesmwa leo na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Agnes Mtawa kwenye kikao kazi cha kuwajengea uwezo wa kusimamia maadili na utendaji kazi wauguzi wakuu wa wilaya kinachoendelea jijini Dodoma.

“Nitoe rai kwa Wauguzi na Wakunga ambao hawajahuisha leseni zao ndani ya miezi sita, sheria inamtaka msajili awafute katika daftari la Uuguzi na Ukunga, na kama watafutwa hawatakuwa na sifa ya uuguzi na ukunga,” amesema Mtawa.

Aidha, Msajili huyo alisema hadi sasa ni asilimia 75 ya wauguzi na wakunga wameshahuisha leseni zao na asilimia 25 waliobaki bado wanaendelea kuangalia kwenda kanzidata yao kwani wapo wauguzi ambao pengine wamefariki, kustaafu na wengine wamebadilisha kada ila kwa wale ambao bado bado wanatoa huduma za uuguzi na ukunga wanakumbushwa kuwa na leseni iliyo kwa mujibu wa sheria ya Uuguzi na Ukunga Namba moja ya mwaka 2010 na kwa wale watakaoshindwa kuhuisha leseni sheria inasema kwamba hawaruhusiwi kuendelea kutoa huduma ya Uuguzi na Ukunga.

“Taarifa imeshapelekwa kwa wahusika na orodha imetayarishwa kwa wale waliohuisha na wale ambao hawajahuhisha watakuwa wamejifuta wenyewe na hawatokuwa na sifa ya kuendelea kutoa huduma za afya na waajiri wao watatakiwa kuwachukulia hatua za kuwafuta kazi kwemye vituo vya umma na vile vya binafsi.

Hata hivyo Bi. Agnes Mtawa aliwakumbusha Wauguzi kuzingatia maadili kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria kwani kumekuwa na malalamiko ya hapa na pale kuhusu utoaji wa huduma kwenye vituo vya afya hivyo kuwakutanisha wauguzi wakuu wa Wilaya kama viongozi na wasimamizi ni chachu katika kukumbushana taratibu na jinsi ya kusimamia miongozo na kanuni.

Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi Kalidushi Charles alisema malalamiko mengi yanaelekezwa kwa wauguzi kwani sehemu kubwa wanaokaa na wagonjwa kwa muda mrefu na ndio watu wa kwanza kupokea wagonjwa hivyo wanapaswa kusimamia sheria, huku akisisitiza kuwa wasioneane haya bali wawajibishane ili huduma za afya ziwe nzuri.

“Tunafahamu sasa hivi serikali ya awamu ya tano imeboresha miundombinu kumekuwa na vituo vingi vya kutolea huduma za afya ambavyo vinafanya upasuaji kwahiyo vituo hivi havitokuwa na maana kama sisi wasimamizi wa hizo huduma hatutosimamia vizuri ili wananchi waweze kupata huduma kama adhma yake Rais” amesema.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Wakuu wa wauguzi ambaye ni Muuguzi kiongozi kutoka Wilaya ya Bukombe Fadhiri Meshack amesema kuwa, mafunzo hayo yanawajengea uwezo viongozi kwa ajili ya kupanua wigo wa uelewa ili kuweza kuwasimamia na kuwasaidia wauguzi wanaowaongoza.