May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Chana: Makumbusho ya Taifa ongezeni kasi

Na Penina Malundo, TimesMajira online

WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Balozi  Dkt.Pindi Chana ameitaka Makumbusho ya   Taifa nchini  kuongeza kasi ya kuhakikisha vituo vidogo vya Makumbusho pamoja na vya Malikale vinaongeza uzalishaji wa mapato tofauti na ilivyo sasa. 

Waziri Chana ameyasema hayo leo alipofanya ziara ya kikazi Kijiji Cha Makumbusho na Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, kwa lengo la kupewa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo na kujionea shughuli mbalimbali za uhifadhi.

Akiwa Kijiji cha Makumbusho, Waziri Chana amesema licha ya kazi nzuri ya uhifadhi wa Utamaduni wa Makabila yatu pamoja na Mazingira lakini ipo haja sasa ya kuongeza ubunifu zaidi wa program  zitakazo toa nafasi kwa watalii kujifunza zaidi ya nyumba zilizopo mfano kuwa na siku ya vyakula vya asili.

“Nachua nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, kwa kutuonesha njia, hivyo kama Wizara tunatakiwa tuitendee haki heshma hii aliyo tupatia kupitia Filamu ya Royal Tour, ninataka kuona na ninyi  Makumbusho ya Taifa mnaitendea haki heshima hii kwa kuboresha maeneo yenu ili watalii waje kujionea Urithi adhimu uliohifadhiwa hapa”amesema  Waziri Chana

Waziri Chana akiwa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam, amejionea uhifadhi mkubwa wa urithi wa vielelezo vya tunu za Taifa kama vile hati ya Uhuru, Vifaa vilivyo tumika kuchangaya udogo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, fuvu la Binadamu wa kale anaesadikika kuishi liaka zaidi ya milioni 1.7 (Zinjanthropus).

Pia Waziri Chana amepata nafasi ya kuona Hifadhi kubwa ya vifaa vya Mila na desturi, matokeo ya tafiti za kibaoloji, maonesho ya Sanaa za kale na za sasa, kupewa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo pamoja na kuzungumza na watumishi.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo, Mkurugenzi Mkuu Wa Makumbusho ya Taifa nchini Dkt Noel Lwoga alitaja mafanikio ni pamoja na ongezeko la watalii hasa kipindi Cha UVIKO 19, mashirikiano mema na wadau mbalimbali hasa katika utafiti na  program za kimakumbusho, kuandaa mpango mkakati wa Shirika 2022/2025, maboresho ya maslai ya watumishi nk

Dkt Lwoga amesema kuwa licha ya mafanikio yaliyopo, Taasisi hiyo inakusudia kuenedea kufanya maboresho Makubwa kwenye Makumbusho zote za Taifa pamoja na Vituo vya Malikale ili kuvutia watalii zaidi wa ndani na wakimataifa.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (RAAWU) Tawi la Makumbusho ya Taifa, Anastasius Liwewa pamoja na kumpongeza Waziri Chana kwa kazi nzuri anazo fanya, alitaja moja ya siri ya mafanikio ya Makumbusho ya Taifa kwa sasa ni uongozi mzuri uliopo unao jali maslai ya watumishi hao pamoja na mkakati mzuri wa kupeleka Taasisi hiyo kwa wananchi zaidi.