August 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kijana abuni mfumo  kuokoa maisha vivuko vya reli


Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Tanga

KIJANA  aliyehitimu katika fani ya Sayansi ya Kompyuta kutoka Taasisi ya Taifa ya Usafirishaji (NIT), Vladimir  Masawe, amebuni mfumo wa teknolojia unaolenga kuzuia ajali katika vivuko vya reli na hivyo kuokoa maisha ya watu.

Masawe alieleza hayo jijini Tanga wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, akisema mfumo huo unaweza kusaidia kudhibiti magari na watumiaji wengine wa barabara pindi treni inapokaribia eneo la kuvuka reli.

Kwa mujibu wa Masawe, mfumo huo unalenga kufanya milango ya kivuko kufungwa kiotomatiki wakati treni inapokaribia na kubaki imefungwa hadi treni inapomaliza kupita. Baada ya treni kuondoka, milango itafunguka na taa za kuongoza magari kubadilika na kutoa ishara ya kuruhusu watumiaji wa barabara kuendelea na safari.

Amesema ubunifu huo umezingatia changamoto zinazoweza kusababisha ajali, ikiwamo hali ya dereva au abiria kuwa ndani ya gari na kusikiliza muziki kwa sauti kubwa kiasi cha kushindwa kusikia honi ya treni inapokaribia.
“Lengo ni kutengeneza mfumo unaoweza kusaidia kuzuia ajali na kuokoa maisha,” amesema Masawe.

Masawe ameiomba Serikali, taasisi na wadau wengine wa usafirishaji kushirikiana naye katika kuendeleza ubunifu huo ili uweze kutekelezwa kwa vitendo katika maeneo yenye changamoto za vivuko vya reli.

Aidha, amezitaka mamlaka husika, ikiwemo Shirika la Reli Tanzania (TRC), kushirikiana na NIT katika kuufanyia kazi ubunifu huo na kuufikisha katika hatua ya utekelezaji.

Amesema ushirikiano huo unaweza kusaidia kuboresha usalama katika maeneo ya vivuko vya reli, huku akisisitiza kuwa mfumo huo ni wazo la kiteknolojia linalolenga kuzuia madhara kabla hayajatokea.

Masawe amesema endapo ubunifu huo utafanikiwa kutekelezwa kwa ufanisi, unaweza kuwa sehemu ya jitihada za kutumia teknolojia katika kupunguza ajali na kulinda maisha ya watumiaji wa barabara hasa kwenyevivuko vya reli.