April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Bashungwa atoa maagizo mazito kwa maafisa elimu Mkoa na wathibiti ubora

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Updates

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Innocent Bashungwa amewaagiza Maafisa wa Elimu wa Mikoa na Wilaya, nchini kuwasimamia Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu wa Masomo, kuzingatia kalenda ya utekelezaji wa mtaala, ili kuwa na ufundishaji na ujifunzaji wenye tija na mahiri.

Akizundua kalenda za utekelezaji wa mitaala na mafunzo kwa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wathibiti Wakuu wa Ubora wa Shule Kanda leo Jijini Dodoma leo Waziri Bashungwa amewaagiza Maafisa Elimu Mikoa, kutoa mafunzo ya matumizi ya Kalenda ya Utekelezaji, katika Halmashauri zenu zote, kabla au ifikapo tarehe 1 Februari, 2022.

Waziri Bashungwa ameitaka Mikoa na Halmashauri, kuwatambua wadau wote wa elimu, waliopo katika maeneo yao na kubaini miradi wanayoitekeleza, kwa kuitembelea na kufanya tathmini ili kuona kama miradi hiyo ina tija katika elimu na kuwaagiza kuhakikisha taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo, iwasilishwe kwa Katibu Mkuu – OR TAMISEMI, kila baada ya miezi mitatu.

Kuhusu Michezo Waziri Bashungwa ameiagiza Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuhakikisha zinasimamia kikamilifu, ratiba ya shughuli za michezo, kwa Shule za Msingi na Sekondari na kuwasisitiza kuzingatia ratiba ya michezo shuleni na kutekelezwa kikamilifu kwa kuwa michezo hutoa fursa kubwa ya kujiburudisha na kujifunza nje ya darasa.

Amewataka Viongozi wa Mikoa, Halmashauri, Kata, Vijiji na wamiliki wa Shule, kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa sera, sheria, miongozo na maelekezo yote ya Serikali, ili kuwe na ufundishaji na ujifunzaji wenye tija na kuwasisitiza kutumia kitabu cha majumuisho ya nyaraka na miongozo ya elimu toleo Namba 1 la Oktoba, 2021, kilichotolewa na OR-TAMISEMI kama rejea katika utekelezaji wa elimu msingi.

Waziri Bashungwa amewaagiza viongozi wa Mikoa , Halmashauri na wakuu wa shule kuhakikisha kutokuwepo na mwanafunzi yeyote wa awali, darasa la kwanza au kidato cha kwanza anatozwa michango kama sharti la mwanafunzi kuandikishwa na kila shule kuhakikisha inakuwa na mwalimu mmoja kwa ajili ya kuandikisha wanafunzi kipindi hiki cha likizo.

“Ninawaagiza Viongozi wote wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa mwongozo wa utoaji wa Elimumsingi Bila Malipo, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameongeza fedha zinazotolewa kila mwezi, kwa ajili ya kugharimia elimu bila malipo, kutoka shilingi bilioni 23 kwa mwezi hadi kufikia bilioni 26 kwa mwezi na niwatake kuendelea kufafanua utekelezaji wa waraka huo kwa wazazi” amesisitiza Waziri Bashungwa

Waziri Bashungwa amewaagiza Maafisa Elimu wa Kata kwa kushirikiana na Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji, kubainisha watoto wote wanaotakiwa kuandikishwa shule wakiwemo watoto wenye mahitaji maalum na kuwasisitiza wazazi kuhusu umuhimu wa kuwaandikisha watoto mashuleni.

Aidha, amewaagiza kuhakikisha wanabandika namba za simu za Kituo cha Huduma kwa Mteja katika kila Ofisi iliyo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, na vituo vyote vya kutolea huduma ikiwemo Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali, Shule, na Ofisi za Watendaji katika ngazi zote.