August 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee watakiwa kuimarisha malezi , maadili ya jamii



Na Mwandishi wetu,Dodoma


SERIKALI imewataka viongozi wa Chama cha Wazee Wanaume Tanzania (CCWWT) kuhakikisha chama hicho kinakuwa chombo muhimu katika malezi, upatanishi, pamoja na utunzaji wa mila, desturi na maadili ya jamii.


Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, wakati wa Mkutano wa Chama cha Wazee Wanaume Tanzania (CCWWT) uliofanyika jijini Dodoma, Agosti 29, 2026.


Profesa Shemdoe amesema wazee ni tunu na hazina ya Taifa kutokana na mchango wao katika malezi, makuzi na ujenzi wa jamii, hivyo wana wajibu wa kurithisha hekima na maarifa yao kwa vizazi vijavyo.


Amesema wazee pia wana nafasi kubwa katika kutoa ushauri, malezi na upatanishi wa migogoro katika jamii, hivyo wanapaswa kuendelea kuwaunganisha wazee wenzao na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.


Aidha, Profesa Shemdoe amesema Serikali inaendelea kutunza na kuwahudumia wazee, ambapo jumla ya wazee 229 wanaishi katika makazi 13 ya wazee yanayomilikiwa na Serikali.


Ameongeza kuwa Serikali pia inatoa huduma za msaada wa kisheria kupitia Mama Samia Legal Aid, kwa lengo la kulinda haki za wazee, ikiwemo haki ya kumiliki mali.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Maryprisca Mahundi, amewahamasisha wazee kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali, ikiwemo mikopo inayoratibiwa na Wizara hiyo kupitia Benki ya NMB.


Amesema mikopo hiyo inaweza kuwawezesha wazee kuanzisha na kuendesha miradi ya maendeleo, kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.


Mahundi pia ametoa wito kwa kila mwananchi kuhakikisha anatimiza wajibu wake wa kulea watoto kwa misingi ya maadili, ili watakapokuwa watu wazima waweze kuishi maisha yenye ustawi na kuwaandalia msingi bora wa uzee wao.


Kwa upande wake, Katibu wa Chama hicho, Flavian Lubuva, amesema lengo la chama ni kuwaunganisha na kuwawezesha wazee kushiriki katika miradi ya maendeleo kwa ajili ya kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.


Ametaja baadhi ya miradi inayotekelezwa na chama hicho kuwa ni ufugaji wa nyuki mkoani Arusha, kilimo cha zabibu jijini Dodoma, pamoja na uvunaji wa nyasi unaolenga kuchangia katika utunzaji wa mazingira.