April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi watakiwa kulipia ada mtihani kidato cha sita mapema

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZAZI wenye wanafunzi wa kidato cha sita wanaotarajia kufanya mtihani wa Taifa mwezi Mei mwaka huu wametakiwa kulipa ada ya mtihani mapema kabla ya kuanza mitihani hiyo ili kuepuka usumbufu wa mtoto kufungiwa matokeo yake .

Akizungumza na Timesmajira online Afisa Uhusiano wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) John Nchimbi amesema,kuchelewa kulipa ada hiyo inasababisha wazazi na walezi kupata usumbufu wa kufuatilia na kulipia ada hiyo Makao Makuu ya NECTA kwa ajili ya kupata matokeo ya watoto wao.

Hata hivyo alisema,hali hiyo inaleta usumbufu kwa NECTA kwa sababu kwa kipindi hicho wanakuwa na shughuli nyingine za muhimu na hivyo kusababisha mzazi au mlezi kutopata matokeo hayo kwa muda alioutarajia yeye.

Vile vile alisema,kadri mzazi  anavyochelewa kulipa ada hiyo ya mtihani ,ndivyo faini inavyozidi kuongezeka kutokana na taratibu zilizowekwa na Baraza hilo.

Nchimbi alisema,kuanzia Julai Mosi hadi Septemba 30 mwaka jana ada hiyo ilikuwa ni shilingi 50,000 lakini kuanzia Oktoba Mosi ada hiyo imepanda kidogo kidogo hadi kufikia 80,000 kwa wale ambao hawajalipa mpaka sasa.

Amesema,kwa wale wazazi ambao watakuwa hawajalipa hadi mitihani itakapoanza ada hiyo itapanda hadi kufikia shilingi 100,000 huku akisema hakuna haja ya wazazi/walezi kufikia huko kwani wanajiongezea gharama na usumbufu wa kuanza kufuatilia matokeo ya mtoto Makao Makuu ya Baraza hilo.

“Tunashauri wazazi/walezi wenye watoto wa darasa la mtihani wanaopaswa kulipia ada hiyo,wafanye hivyo mapema kabla ya faini kuanza kupanda ..,hii ni gharama nyingine kwa mzazi,

“Lakini pia kulipa mapema inarahisisha kwani matokeo ya mtoto yanapatikana bila usumbufu wowote pindi matokeo yanapotangazwa,lakini mzazi akisubiri mpaka mitihani inapoanza analipa gharama kubwa lakini pia kuna kufungiwa matokeo ambayo itamlazimu mzazi kuanza kufunguliwa kwa matokeo hayo.”amesema Nchimbi

Ametumia fursa hiyo kuwasihi wakuu wa shule kuwahimiza wazazi kulipia ada hiyo mapema kwa kutumia njia zozote wanazoona zinaweza kuwafikia ili kuwaondolea usumbufu ambao utajitokeza baadaye.

“Taarifa hizi za ada ya mtihani hadi faini zake huwa tunazifikisha shuleni tukitarajia Wakuu wa shule wanazifikisha kwa wazazi,tunawasihi wazingatie kutoa taarifa hizi ili wazazi/walezi wenye watoto walio kidato cha mtihani wa Taifa wachukue hatua mapema.”amesisitiza Nchimbi