May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi wahimizwa kuhamasisha masomo ya sayansi

Na Queen Lema,Timesmajira Online,Arusha

Wazazi pamoja na walezi nchini hapa wamehimizwa kuwahamasisha na kiwajenge watoto wa kike msingi mzuri wa kufanya bidiii katika masomo ya sayansi ambapo kwa kufanya hivyo kutaweza kuwaruhusu kuweza kuingia rasmi kwenye sekta ya usafiri wa anga.

Hayo yameelezwa jijini Arusha na Godlove Longole ambaye ni Mkufunzi kutoka katika Chuo cha Civil Aviation Training Centre kilichopo jijini Dar es Salaam wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye mkutano wa wadau wa usafirishaji unaoendelea mkoani humo.

Godlove amesema kuwa ndani ya sekta ya anga kuna vigezo ambavyo vinaangaliwa ikiwepo ufaulu mzuri hasa wa masomo hayo ya Sayansi.

Hivyo endapo wazazi watahakikisha kuwa tangu awali watoto wa kike wanajifunza masomo ya sayansi itaweza kuwarahisishia uwezo wa kupata nafasi ya kujifunza lakini pia kusoma masomo ya anga.

“katika uchaguzi kwenye fani hii hatuangalii uwezo wa kuongea au kujiamini kwa mtoto wa kike badala yake tunaangalia ufaulu hasa wa masomo ya Sayansi hivyo basi ni muhimu sana kwa jamii kuhakikisha kuwa wanayafuatilia vyema masomo hayo,”.

Wakati huo huo amesema kuwa chuo hicho kinatarajia kuweka mikakati mbalimbali ambayo itachangia kumpa ari mtoto wa kike kuweza kupenda sekta ya anga.

“hawa watoto wa kike ambao wapo katika fani hii jamii yenyewe ni mashaidi jinsi ambavyo wanakuwa na umakini mkubwa sana kwenye kazi na fani yao sasa tutaaangalia namna ya kuwapa ari na motisha ili waweze kufika mbali zaidi,”amesema.

Hata hivyo amewataka Watanzania kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo ndani ya chuo ili kuweza kupata mafunzo kwa fani hiyo ambayo bado inahitaji wataalamu.